Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Zainab Telack amefanya ziara ya kutembelea miradi ya maji katika Wilaya ya Kishapu leo Machi 03, 2021 ambapo amekagua miradi hiyo katika vijiji 06 vikiwemo vijiji vya Bubiki, Bubiki B, Ukenyenge, Mayanji, Negezi na Bulimba.
Katika ziara hiyo Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) ambao wamepewa jukumu la kusimamia Sekta ya Maji Vijijini ikiwemo ujenzi wa miradi ya maji na utoaji wa huduma ya maji wamekabidhi miradi hiyo ya maji itakayohudumia idadi ya wakazi wapatao 192,517 kupitia mradi wa awamu hii katika wilaya ya Kishapu.
Kupitia utekelezaji wa programu ya maji ya P4R kwa mwaka wa fedha 2020/2021, RUWASA Kishapu imepata kiasi cha Tsh 2.8 Bilioni ambapo itaendelea na ujenzi wa miradi ya maji katika vijiji vya Mwangongo, Ndoleleji, Lagana/Mihama, Nyasamba, Uchunga/Kakola.
Mkuu wa Mkoa Bi. Zainab Telack amewapongeza RUWASA kwa kukamilisha ujenzi wa miradi ya maji na wananchi kupata huduma huku akiwataka wananchi kutunza miradi hiyo ya maji katika maeneo yao na kutoa taarifa za uharibifu kwenye vyombo vya usalama.
“Nawapongeza RUWASA kwa kukamilisha miradi hii ya maji na kufikisha huduma kwa wananchi, navyi wananchi hakikisheni mnalinda hii miradi kwa ufanisi” amesema Telack.
Naye Ndamba Masiya ambaye ni mjumbe wa Jumuiya za Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii ameishukuru serikali ya awamu wa tano kwa kutimiza ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya kuwaletea maji safi na salama katika vijiji vyao na kumtua mama ndoo kichwani ambapo imepelekea kuepuka usumbufu wa kufuata maji umbali mrefu.
“Sisi akina mama tulikuwa tunapata migogoro ndani ya familia zetu na usumbufu wa kufuata maji umbali mrefu ambayo pia siyo salama kwa afya ya familia zetu. Tunaipongeza sana serikali yetu kwa kutimiza ahadi kwa wananchi wake” amesema Masiya.
Katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama na yenye kutosheleza maeneo ya vijijini na Mji mdogo wa Wilaya ya Kishapu, RUWASA imejikita katika ukarabati wa visima na miradi ya maji yenye kuleta matokeo ya haraka, kuongeza upatikanaji wa maji na imefanikiwa kumtua mama ndoo kichwani kuelekea ‘Siku ya Wanawake Duniani’ Machi 08, 2021.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa