Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mh. Nyabaganga Taraba ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya hiyo kuwahamasisha wananchi hususan wawekezaji wadogo kujenga viwanda vidogo vidogo.
Pia ameitaka kujenga mazingira bora na wezeshi kwa ajili ya kuwapa fursa wawekezaji wadogo wadogo ili kutimizia azma ya kuwa na wilaya ya viwanda.
Mh. Taraba alitoa rai hiyo wakati wa kikao na uongozi wa Halmashauri ya Kishapu cha kujadili namna ya kuibua fursa za uwekezaji wa viwanda vidogo vidogo wilayani humo ili kuendana na kasi ya sera ya nchi ya viwanda.
Alisema wawekezaji wadogo wana nafasi yao na hivyo wanapaswa kutiwa moyo na kutokatishwa tamaa katika hatua zao za kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali katika wilaya hiyo.
Mkuu huyo wa wilaya aliongeza kwa kufafanua kuwa dhana ya viwanda si lazima viwe vikubwa katika majengo makubwa bali ni pamoja na vile vidogo vye kuzalisha bidhaa kwa wananchi.
Pia aliagiza watumishi katika idara ya maendeleo ya jamii kwenye Halmashauri hiyo kuwa karibu na wananchi wenye nia na kufanya uwekezaji kwa kuwahamasisha kujenga viwanda vidogo vidogo.
Aidha alitaka visiwepo vikwazo kwa wananchi na hivyo kuweza kuchangia kuzorota katika kazi ya kujenga viwanda bali tuwashike mkono katika kutimiza azma yao ya kujenga uchumi wa viwanda.
Alishauri Halmashauri itenge fedha kwa ajili ya kuwakopesha wananchi wenye nia ya kuanzisha viwanda na kisha watakaposimama waweze kurudisha mikopo hiyo ili isaidie vikundi vingine.
Wakichangia katika kikao hicho Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Alphonce Bagambabyaki alitaka yatengwe maeneo madogo kwa ajili ya kuwavutia wawekezaji wadogo.
Alisema dhana ya viwanda si lazima iwe maeneo makubwa ya kujenga viwanda vikubwa lakini inawezekana pakawa na vikundi vidogo au mtu mmoja mmoja anayeweza kuwa na kiwanda kidogo.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Katibu Tawala Wilaya, Shadrack Kengese, Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Stephen Magoiga na wakuu wa idara na vitengo.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa