Na Ofisi ya Habari, Kishapu
Mkuu wa wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Mheshimiwa Nyabaganga Taraba amesema zoezi la utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa ng’ombe kwa kutumia chapa litapunguza changamoto zinazowakabili wafugaji.
Alisema hayo jana wilayani hapa wakati akiongoza kikao cha maofisa mifugo pamoja na watendaji kata na vijiji kwa ajili ya kuhamasisha zoezi hilo linalotarajiwa kuanza Agosti 28 mwaka huu.
Mh. Taraba alibainisha kuwa Kishapu ni miongoni mwa wilaya ambazo baadhi ya wafugaji wake wanakabiliwa na matatizo yakiwemo wizi wa mifugo, migogoro na magonjwa hivyo zoezi hili litasaidia kuyapunguza.
Aidha aliwataka wataalamu wa mifugo na watendaji hao kufanya kazi kwa ushirikiano ili kufanikisha zoezi hilo ambalo linatarajiwa kufanyika vijiji vyote vya wilaya hiyo vyenye mifugo.
“Maofisa mifugo hakikisheni mnafanikisha zoezi hili siyo kusubiri ratiba hakuna atakayekusimamia na kazi lazima ziende ng’ombe anaugua wakati wowote na unapaswa kuwa tayari wakati wowote.
“Tunataka Kishapu tuwe mfano kwa kulifanikisha zoezi hili muhimu na nyie maofisa mifugo muwaelekeze watendaji wenu pale mnapokwamba muwasiliane na ofisi ya mkurugenzi watawasaidia,” alisisitiza.
Kwa upande wake Ofisa Mifugo na Maendeleo ya Mifugo wa halmashauri ya wilaya hiyo, Dk. Aphonce Bagambabyaki aliwataka wataalamu hao kutumia taaluma zao kutoa elimu kwa wafugaji kuhusu umuhimu wa utambuzi na usajili wa ng’ombe.
Alisema hilo ni agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambalo linataka mifugo yote nchini kutambuliwa kwa kutumia chapa chini ya sheria ya utambuzi namba 12 sura namba 184.
Kaulimbiu yake ni sajili mifugo yako kwa uhakika wa soko na udhibiti wa wizi wa mifugo ambapo Dk. Bagambabyaki alisema mfumo utakaotumika ni alama ya moto inayopigwa kwenye ng’ombe ambapo chapa hiyo itawekwa mguu wa nyuma juu ya goti.
“Endapo mfugaji ataweka alama binafsi atapaswa kuweka upande wa mkono wa kulia chini ya kiwiko na iwe imesajiliwa kwa kuzingatia kanuni ya tisa ya usajili wa mifugo.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa