Elimu ya homa kali ya mapafu yazidi kutolewa kwa jamii ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kupitia Timu ya Majanga ya Afya Kishapu imetoa elimu hio ya tahadhari ya Mlipuko wa Ugonjwa wa Homa ya Mapafu inayosababishwa na Kirusi aina ya Corona katika Mgodi wa Williamson uliopo kata ya Mwadui Luhumbo wilaya Kishapu mkoani Shinyanga.
Imeelezwa kuwa Shirika la Afya Duniani (WHO) liliutangaza ugonjwa huo kuwa ni dharura ya kimataifa, tarehe 31 Desemba 2019 iliripoti juu ya kuwepo kwa Kirusi aina ya Corona katika mji wa Wuhan huko China ambako ndio kitovu cha ugonjwa huo. Wiki moja baadaye serikali ya China ilithibitisha kuwepo kwa Kirusi hicho kipya aina ya ‘coronavirus’ kilichopewa jina la COVID-19 (Corona Virus Disease 2019) hadi sasa ugonjwa huu umeripotiwa kusambaa katika nchi 190 ikiwemo China yenyewe.
Aidha ripoti ya WHO hadi kufikia tarehe 23 March 2020 wamethibitisha kuwa watu zaidi ya 33,981 wameugua ugonjwa wa Corona huku idadi ikiongezeka kwa kasi na waliothibitika kufariki ni zaidi ya watu 14,652. Hadi sasa ugonjwa wa Corona hauna chanjo wala tiba, hivyo mgonjwa anatibiwa kutokana na dalili alizo nazo na uchunguzi unaendelea.
Kwa Tanzania hadi sasa kuna jumla idadi ya wagonjwa wa Corona 12 ambapo nane kati yao ni raia wa Tanzania na wengine wanne ni raia wa kigeni. Ugonjwa huu kwa Tanzania haujaripotiwa kuua mtu hata mmoja. Katika juhudi za kudhibiti kuenea kwa maambukizi wageni wote wanaoingia nchini kutoka katika mataifa yaliyoripotiwa kuwa na ugonjwa huo watatengwa kwa siku 14. Aidha agizo hilo lililotolewa na Raisi wa Jamuhuri wa Muungano wa Tanzania,John Pombe Magufuli linawajumuisha Watanzania wanaorejea nyumbani kutoka nchi nyingine.
Hatua nyingine zilizochukuliwa kuthibiti ugonjwa huu ni pamoja na kufunga shule zote kwa muda wa siku 30 pamoja na kuzuia mikusanyiko yote ya watu wengi yakiwemo matamasha ya mziki,mikutano ya hadhara mbalimbali ikiwemo ya kisiasa.
Akizungumza wakati wa kutoa elimu hio, Afisa Afya wa Wilaya ya Kishapu, Erick Yossam Muhigi alieleza namna ya kuchukua tahadhari na kujikinga na ‘covid-19’ huku akisisitiza usafi binafsi kwa kila mtu huku kila mmoja akiwa ni balozi wa mwenzake kwa usafi.
“kutokana na mwingiliano wa watu kutoka mikoa ya pembezoni mwa nchi na pia wasafiri kutoka nchi mbalimbali tunapaswa kuchukua tahadhari hasa kwa watu wenye dalili za ugonjwa huu kama vile matatizo katika mfumo wa hewa ikiambatana na homa kali, kukohoa, vidonda kooni, kubanwa mbavu, mwili kuchoka, maumivu ya misuli na mafua makali. Ambapo inaaminika dalili za ugonjwa huonekana siku 1-14 baada ya mtu kuambukizwa” alisema Muhigi.
“Kuimarisha usafi kwa kunawa mikono kwa maji safi tiririka na sabuni mara kwa mara au kutumia hand sanitizers kwa kuchanganya glycerine na spirit,ambapo kwa ujazo wa lita moja ya spirit unaweka vifuniko viwili vya glycerine, funika mdomo na pua wakati wote wa kukohoa au kupiga chafya. Kwa kuwa virusi vya ‘Covid2019’ vina ukubwa wa 400-500 Micro hivyo kwa kutumia kitambaa au mikono safi unaweza kuzuia virusi hivi, kuepuka kugusana na mwenye dalili za Corona, kutupa vifaa vilivyotumika kama masks na hand sanitizers katika chombo cha kuhifadhia taka, kusafisha kwa kutumia dawa ya kuua vijidudu kwenye vitasa vya milango, sakafu na nguo za wagonjwa, epuka kugusa pua, macho na mdomo kwa mikono isiyo safi, kuepuka kuwa karibu sana na watu wenye Corona, hizi zitachangia kwa kiasi kikubwa kuepuka ugonjwa wa Corona” aliongeza Muhigi.
Timu ya Afya ya Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kwa kushirikiana na timu ya kukabiliana na majanga imejiandaa kukabiliana na homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi aina ya Corona imetenga Kituo cha Afya cha Kishapu kilichopo wilayani Kishapu kama eneo la kuhudumia wagonjwa wa Corona. Aidha timu imeandaa magari na mafuta kwa ajili kuwezesha shughuli za uratibu na ufuatiliaji. Pia Halmashauri inaendelea kutumia mfumo uliopo wa Ufuatiliaji na Uthibiti wa Magonjwa (IDSR) katika kubaini washukiwa wa ugonjwa wa Corona. Timu ya Afya Wilayani Kishapu imeagiza dawa na vifaa tiba muhimu kwa ajili ya kutibu dalili za ugonjwa huu. Kuandaa na kuwezesha mafunzo kwa watumishi wa Afya na wanajamii juu ya ugonjwa wa Corona. Mkuu wa Wilaya ya Kishapu
Naye Mhandisi Mkuu wa Mgodi wa Williamson Mwadui, Injinia Shagembe Mirawa alitoa wito kwa kwa wafanyakazi wote wa mgodi hu kuchukua tahadhari kama walivyoelezewa na aAfisa Afya.
“kampuni imechukua hatua za awali kama kuandaa vifaa vya kunawa mikono kwenye maeneo yote ya mgodi pia getini kuna ‘thermo Scanner’ kwa ajili ya kupima hali joto kwa kila mtu anaye ingia mgodini pia tusaidie familia zetu kwa kuwapa elimu na kuweka ratiba ya kunawa mikono majumani mwetu, sisi kama wafanya kazi tuungane na juhudi hizi za kujikinga thidi ya ugonjwa huu na tusidharau” alisema Mirawa.
Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kama vile Viongozi wa dini, Msalaba Mwekundu na NGO’S wamejipanga kutoa elimu juu ya ‘covid2019’ kwa jamii kama vipaza sauti vya magari katika maeneo mbalimbali, nyumba za ibada, minada katika katika wilaya ya kishapu.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa