Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga imetoa elimu ya tahadhari ya Mlipuko wa Ugonjwa wa Homa ya Mapafu inayosababishwa na Kirusi aina ya Corona.
Imeelezwa kuwa Shirika la Afya Duniani (WHO) tarehe 31 Desemba 2019 iliripoti juu ya kuwepo kwa Kirusi aina ya Corona katika mji wa Wuhan huko China. Wiki moja baadaye serikali ya China ilithibitisha kuwepo kwa Kirusi hicho kipya aina ya ‘coronavirus’ kilichopewa jina la COVID-19 (Corona Virus Disease 2019) hadi sasa ugonjwa huu umeripotiwa kusambaa katika nchi 109 ikiwemo China yenyewe.
Aidha WHO wamethibitisha kuwa watu zaidi ya 113,702 wameugua ugonjwa wa Corona huku idadi ikiongezeka kwa kasi na waliothibitika kufariki ni zaidi ya watu 563. Hadi sasa ugonjwa wa Corona hauna chanjo wala tiba, hivyo mgonjwa anatibiwa kutokana na dalili alizo nazo na uchunguzi unaendelea.
Akizungumza wakati wa kutoa elimu hio, Afisa Afya wa Wilaya ya Kishapu, Erick Yossam Muhigi alieleza namna ya kuchukua tahadhari na kujikinga na ‘covid-19’ huku akisisitiza usafi binafsi kwa kila mtu huku kila mmoja akiwa ni balozi wa mwenzake kwa usafi.
“kutokana na mwingiliano wa watu kutoka mikoa ya pembezoni mwa nchi na pia wasafiri kutoka nchi mbalimbali tunapaswa kuchukua tahadhari hasa kwa watu wenye dalili za ugonjwa huu kama vile matatizo katika mfumo wa hewa ikiambatana na homa kali, kukohoa, vidonda kooni, kubanwa mbavu, mwili kuchoka, maumivu ya misuli na mafua makali. Ambapo inaaminika dalili za ugonjwa huonekana siku 1-14 baada ya mtu kuambukizwa” alisema Muhigi.
Kuimarisha usafi kwa kunawa mikono kwa maji safi tiririka na sabuni mara kwa mara au kutumia hand sanitizers, funika mdomo na pua wakati huo wa kati wote wa kukohoa au kupiga chafya. Kwa kuwa virusi vya ‘Covid2019’ vina ukubwa wa 400-500 Micro hivyo kwa kutumia kitambaa au mikono safi unaweza kuzuia virusi hivi, kuepuka kugusana na mwenye dalili za Corona, kutupa vifaa vilivyotumika kama masks na hand sanitizers katika chombo cha kuhifadhia taka, kusafisha kwa kutumia dawa ya kuua vijidudu kwenye vitasa vya milango, sakafu na nguo za wagonjwa, epuka kugusa pua, macho na mdomo kwa mikono isiyo safi, kuepuka kuwa karibu sana na watu wenye Corona, hizi zitachangia kwa kiasi kikubwa kuepuka ugonjwa wa Corona” aliongeza Muhigi.
Timu ya Afya ya Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kwa kushirikiana na timu ya kukabiliana na majanga imejiandaa kukabiliana na homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi aina ya Corona imetenga Kituo cha Afya cha Kishapu kilichopo wilayani Kishapu kama eneo la kuhudumia wagonjwa wa Corona. Aidha timu imeandaa garari na mafuta kwa ajili kuwezesha shughuli za uratibu na ufuatiliaji. Pia Halmashauri inaendelea kutumia mfumo uliopo wa Ufuatiliaji na Uthibiti wa Magonjwa (IDSR) katika kubaini washukiwa wa ugonjwa wa Corona. Timu ya Afya Wilayani Kishapu imeagiza dawa na vifaa tiba muhimu kwa ajili ya kutibu dalili za ugonjwa huu. Kuandaa na kuwezesha mafunzo kwa watumishi wa Afya na wanajamii juu ya ugonjwa wa Corona.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mheshimiwa Nyabanganga Taraba alitoa wito kwa timu ya kukabiliana na majanga wilayani Kishapu kukuchukua tahadhari mapema kwa vitendo pia kwa wazazi na walezi juu ya elimu hii kwa watoto wao ili kujikinga na janga hili.
“Haya yaliyozungumzwa hapa tuyazingatie, timu ya kukabiliana na majanga naomba tuweke mikakati na kutoa elimu kwa jami, tuache kusalimiana kwa kushikana mikono, tuwape elimu watoto wetu wakiwa shuleni watakuwa mabalozi wazuri kwa wengine, hivyo tuwe mabalozi kuwabaini wagonjwa na kutoa taarifa sehemu husika” alisema Taraba
Kadhalika, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Dr. Josephat Shani alitoa tahadhari kwa wanajamii kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima kwa kuwa huu ugonjwa unaenea kwa haraka hivyo tujikinge tusiambukizwe ambapo kwa bara la Afrika tayari kuna baadhi ya nchi zina ugonjwa wa Corona.
Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kama vile Viongozi wa dini, Msalaba Mwekundu na NGO’S wamejipanga kutoa elimu juu ya ‘covid2019’ kwa jamii kupitia mikusanyiko kama nyumba za ibada, minada na semina katika maeneo mbalibmali katika wilaya ya kishapu.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa