Ikiwa ni baada ya miaka mitano ya utendaji kazi, Good Neighbors wakabidhi mradi waliokuwa wanaufanya wa kuboresha afya ya uzazi kwa wanawake wajawazito na watoto. Mradi ulilenga kuwawezesha wahudumu wa afya katika vituo vya afya takribani 49 wilayani Kishapu. Good Neighbors katika utekelezaji wa huduma ya mama na mtoto wilayani Kishapu ilianza mwaka 2015 hadi 2018 na kuongeza mwaka mmoja 2019 ikiwa na lengo la kufuatilia kwa ukaribu kile ambacho walikianzisha huku kauli mbiu ya mradi huu ikiwa ni " afya ya uzazi kwa wote" ikimaanisha kwa pamoja kama wana Kishapu tuungane kuhakikisha mama na mtoto wanapata huduma bora kwa wakati.
Akiongea katika makabidhiano hayo Mkurugenzi Mkazi wa Good Neighbors Bwana Hunggoo Ann amewashukuru sana wanajamii, madaktari na wauguzi katika hospitali na zahanati zote kwa kushirikiana nao kuhakikisha mradi huo unakamilika huku mama na mtoto wakipata huduma bora. Pia amewaasa wanajamii kuzidi kushirikiana ili kuhakikisha miundombinu na vifaa vyote walivyovikabidhi vinakuwa katika hali ya ubora ili kuwa msaada kwa jamii.
Katika makabidhiano hayo, Good Neighbors walifanikiwa kukabidhi miundombinu kama nyumba za wahudumu, wodi za wazazi na vifaa kama vile, magari 3, jenereta 2, simtank 1, kompyuta 4, pikipiki 1, copying machine 1, printers 2, speakers 2, screen projectors 2, photo printers 2, viti, USB hard disk, na kamera.
Naye mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Bi. Nyabaganga Taraba, wakati wa makabidhiano hayo aliwashukuru Good Neighbors kwa kuwa mradi umekuwa na manufaa makubwa kwa Wanakishapu kwa kuwa idadi ya wajawazito wanaokwenda kliniki wakati mimba ikiwa chini ya wiki 12 huku wakisindikizwa na waume zao imeongezeka, huku vifo vya wa watoto wachanga vimepungua sana kwani jamii imeelewa juu ya afya ya uzazi. Pia Mkuu huyo wa Wilaya aliwaomba Good Neighbors kuendelea kushirikiana na wana Kishapu kwa kuhamia kwenye mradi mwingine wa maendeleo, kama elimu.
Aidha mganga mkuu wa wilaya ya Kishapu Dr.Shani Josephat Mudamu alitoa takwimu juu ya afya ya mama na mtoto kuwa kuna ongezeko la mahudhurio ya kliniki kwa wajawazito mimba ikiwa chini ya wiki 12 kwa mwaka 2015 hadi 2018 kutoka 0 hadi 11064. Pia wajawazito waliopima wingi wa damu na kuzuia kaswende iliongezeka baada ya kupata elimu kutoka Good Neighbors. hali hio imepelekea wajawazito kujifungua kwenye vituo vya afya salama na kupunguza vifo vya watoto wachanga kutoka watoto 76 kupungua hadi watoto 26 kwa mwaka 2015 hadi mwaka 2018.
Naye mhudumu wa afya ngazi ya jamii Bi. Zubeda ambaye ni mfawidhi wa kituo cha afya zahanati ya Mipa ameeleza kunufaika na mradi huu wa Good Neighbors kwani kupitia elimu wanayoitoa kwa jamii, wajawazito wanajifungua salama katika vituo vya afya tofauti na awali ambapo walikuwa hawana elimu juu ya afya na kupelekea kujifungulia nyumbani na kupelekea matatizo ya kiafya kwa mama na mtoto.
Good Neighbors wamefanikiwa kuongeza uelewa kwa jamii juu ya afya ya uzazi pia ongezeko la utayari kwa wahudumu wa afya kutoa huduma bora kwa jamii. Nao wanakamati ngazi ya jamii wamafanikiwa kutengeneza sheria ndogondogo zakuwabana wanajamii juu ya afya ya uzazi.
Na Catherine J. Ngowi
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa