Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kwa kushirikiana na wadau wa elimu imetatua changamoto zinazoikabili sekta hiyo kwa kuwekeza katika usafiri kwa maafisa elimu kata.
Itakumbukwa Serikali kupitia Programu ya Uboreshaji wa Elimu Tanzania iliwapatia pikipiki maofisa elimu kata zote 29 katika wilaya hiyo ambayo imesaidia kuboresha sekta hiyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, maofisa elimu kata hao walisema kuwa na usafiri huo kumesaidia kuleta ufanisi katika majukumu yao na kuwa ufaulu umeongezeka.
Walisema hivi sasa wanaweza kuzunguka na kukagua shule nyingi kwa kipindi kifupi tofauti na zamani ambapo walitumia zaidi ya wiki mbili kukagua shule chache.
Aidha walibainisha kuwa pikipiki zimewasaidia kuwasilisha taarifa wilayani kwa urahisi na kwa wakati na pia zimewapunguzia gharama ya usafiri ambapo awali walitumia mishahara yao kulipia nauli.
Ofisa Elimu Vifaa na Takwimu, Richard Mutatina alisema kazi ya ukusanyaji takwimu kutoka shule mbalimbali umerahisishwa kwani ofisa elimu kata akihitajika anawasilisha kwa wakati.
Hata hivyo bado kuna changamoto mbalimbali zinazokabili sekta hiyo zikiwemo baadhi ya wananchi kutokuwa na mwamko wa elimu ambapo wanaona ni kama kupoteza muda.
Kwa mujibu wa Ofisa Elimu Taaluma, Emmanuel Ngobai bado wapo baadhi ya wazazi wanawazuia watoto wao kufanya vizuri katika mitihani yao ili wawaingize katika shughuli za kilimo na ufugaji.
Aliongeza kuwa ipo changamoto nyingine kwa baadhi ya walimu kuomba ruhusa mara kwa mara pasipo na mpangilio hali inayosabisha wanafunzi kutopata wasaa mzuri wa kupata vipindi.
Ngobai alisema Halmashauri kupitia Idara ya Elimu Msingi imeweka utaratibu maalumu ambapo maofisa elimu kata wanafanya ukaguzi wa mara kwa mara wa kushtukiza.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa