Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu imefanya tathmini ya zoezi la upigaji chapa ng’ombe ambalo lilizinduliwa Septemba 9 mwaka jana na Mkuu wa Wilaya, Mhe. Nyabaganga Taraba.
Katika tathmini hiyo imeweza kutambua, kusajili na kupiga chapa jumla ya ng’ombe 225,894 ambao ni sawa na asilimia 75 ya lengo la ng’ombe 330,000 iliyokuwa imejiwekea.
Akizungumza na maafisa mifugo na watendaji kutoka kata mbalimbali wilayani humo zilizohusika katika zoezi hilo, Mhe. Taraba alitaka zichukuliwe hatua kwa wafugaji wanaokataa kutoa ushirikiano.
Akiwapongeza kwa kufanikisha alisema kuwa hilo ni zoezi endelevu na litafanyika tena ili kuhakikisha ng’ombe wote wanafikiwa na kutambuliwa kwani kuna ng’ombe ambao hawajapigwa chapa kutokana na sababu mbalimbali.
“Hatukuweza kuwafikia ng’ombe wote kwa mfano kule Magalata wakati tunapita ng’ombe walikuwa wamehamia mbugani malishoni sasa kwa vile mvua zimeanza nina imani watarudi hivyo tutawafikia awamu ya pili,” alisema.
Mhe. Taraba alitaja changamoto nyingine kuwa ni muitikio mdogo wa wananchi katika zoezi hilo na kuwa kata ya Mwamalasa pamoja na kuonekana kuwa na ng’ombe wengi lakini bado ni wachache waliopigwa chapa.
Awali akiwasilisha taarifa yake, Mratibu wa zoezi, Farles Mwenura alisema ili kukabiliana na changamoto hizo Serikali za vijiji ziainishe majina ya wafugaji wakorofi na kuwachukulia hatua.
Pia maafisa ugani wasimamie wafugaji kwa makini wakati wa upigaji chapa ili kuepusha uwezekano wa vidonda kutokea, kutopiga chapa wakati wa mvua na pia kutokandamiza sana chuma kwenye ngozi.
Itakumbukwa kuwa zoezi hili ni agizo la Mheshimiwa Waziri Mkuu na liko chini yasheria namba 12 sura ya 184 linalotaka mifugo yote kutambuliwa kwa kutumia chapa ya moto.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa