Kamati ya Fedha, Utawala na Mipango katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga imeridhishwa na kupongeza hatua ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Hayo yamejiri leo wakati ikifanya ziara ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotekelezwa katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2018/2019.
Wajumbe wa Kamati hiyo wakiongozwa na Diwani wa kata ya Bunambiyu, Mhe. Richard Sangisangi aliyemwakilisha mwenyekiti wa kamati hiyo walijionea hatua za ujenzi wa vyumba vya madarasa katika kata ya Talaga.
Katika shule ya msingi Jijongo iliyopo kwenye kata hiyo walikagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba vinne na ofisi moja ya walimu mradi ambao mbali ya kutekelezwa na Serikali pia nguvu za wananchi zimechangiwa.
Kukamilika kwa miundombinu hiyo ya kutasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa na hivyo kutekeleza kwa ufanisi sera ya elimu bila malipo.
Pia kamati hiyo ilitembelea mradi wa vikundi vya wanawake katika kata ya Songwa ambao unafadhiliwa na Halmashauri kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii kwa kutumia mapato yake ya ndani.
Fedha hizo zinazotolewa kwa kikundi hicho ni sehemu ya asilimia 10 zinazotolewa pia kwa vijana na watu wenye ulemavu kama ambavyo Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu inavyotekeleza.
Katika kufuatilia kama fedha zinazotolewa na Serikali kwa walengwa kaya maskini kwa ufadhili wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Kamati ilimtembelea mnufaika Veronica Mapapala mkazi wa Mhunze.
Mlengwa huyo katika kumfuatilia ameonesha mafanikio kwa kuboresha makazi yake ambapo amejenha nyumba ya bati tofauti na awali ambapo aliishi kwenye tembe lililoezekwa kwa nyasi.
Aidha, miradi mingine iliyotembelewa ni pamoja na ule wa stendi kubwa ya mabasi katika eneo la Maganzo ambalo kukamilika kwake itakuwa chanzo kikubwa cha mapato kwa Halmashauri.
Mradi mwingine ni ule wa upimaji wa viwanja katika eneo hilo la Maganzo ambapo Halmashauri inatarajiwa kuanza zoezi la uuzaji kwa wananchi kwa ajili ya shughuli mbalimbali.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa