Na Ofisi ya Habari, Kishapu
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Amour Hamad Amour amewataka Watanzania kuepuka utumwa wa kutegemea kununua bidhaa kutoka nje ya nchi.
Ametoa mwito huo mwanzoni mwa wiki wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru wilayani Kishapu mkoa wa Shinyanga alipoweka jiwe la msingi kuzindua miradi mbalimbali wilayani humo.
Mwenge wa Uhuru 2017 ukiwa na kaulimbiu ‘Shiriki kukuza uchumi wa viwanda kwa maendeleo ya nchi yetu’ ulizindua miradi mbalimbali ya maendeleo.
Miradi hiyo ni mashine za kusindika mafuta ya alizeti, unga wa mahindi pamoja na mashine ya kukoboa mpunga na kuweka kuweka viwango vya madaraja, Amour alitaka inufaishe wananchi.
Alisema sasa wakati umefika kwa Watanzania wawe wa kwanza kununua bidhaa hizo ili wawekezaji hao wapate kipato na kulipa kodi serikalini kupitia halmashauri.
Miradi hiyo yenye thamani ya sh. milioni 244 unaomilikiwa na mjasiliamali Nassoro Salum na mradi mwingine wa mjasiliamali Mabela Masolwa wenye thamani ya sh. milioni 535.9 kwa pamoja italeta manufaa kwa wananchi wa wilaya hiyo.
Amour alibainisha kuwa viwanda hivyo vidogo vitakuwa chachu ya maendeleo na vitamsaidia mkulima kuzalisha mazao kwa wingi kwa ajili ya malighafi. Viwanda hivi vitaweza kuzalisha ajira kwa wananchi.
“Watalaamu wa kilimo wawaongezee ujuzi wakulima ili kupata malighafi nyingi kwa ajili ya viwanda ambavyo sasa vinaongeza thamani ya mazao kupitia bidhaa vinazozalisha na tutegemee kununua mchele, unga na mafuta ya alizeti hapa nchi na siyo kutegmea nje,” alisisitiza Amour.
Aidha, alipongeza halmashauri ya wilaya hiyo kwa kutenga eneo rasmi la viwanda lenye ukubwa wa ekari 278 katika mji mdogo wa kishapu ambalo thamani yake ni sh. bilioni 1.1.
Kiongozi huyo aliwataka wawekezaji wanaotarajiwa kujenga viwanda katika eneo hilo kutoa kipaumbele cha ajira kwa wakazi wa wilaya ya Kishapu.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa