Na Ofisi ya Habari, Kishapu
Halmashauri ya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga imeng’ara na kushinda nafasi ya tatu kati ya halmashauri zote za mikoa ya Kanda Ziwa zilizoshiriki maonesho ya Sikukuu ya Wakulima (Nanenane).
Katika maonesho hayo yaliyofanyika kwa siku takriban saba viwanja vya Nyamhongolo mkoani Mwanza yalishirikisha halmashauri zote za mikoa sita ikiwemo Shinyanga, Mwanza, Geita, Simiyu, Mara na Kagera.
Kishapu ilizawadiwa kikombe na cheti cha Maonesho hayo hayo ambayo kwa mwaka huu yakiwa na kaulimbiu ‘Zalisha kwa tija mazao na bidhaa za kilimo, mifugo na uvuvi ili kufikia uchumi wa kati’.
Katika banda la halmashauri hiyo wananchi waliotembelea walijionea na kupata elimu ya ufugaji bora wa kuku kutoka kwa maofisa mifugo.
Sambamba na hilo waliweza pia kuona namna ya ufugaji bora wa nyuki pamoja na mchakato wote wa kurina asali kutoka kwa wataalamu na wafugaji wa nyuki.
Si hiyo tu pia vivutio vingine katika banda hilo ilikuwa ni kiwanda kidogo cha bidhaa za ngozi maarufu wilayani Kishapu cha Badimi pamoja na namna ya ufumaji wa mazulia kutokana na zao la mkonge.
Wananchi walipata elimu ya usindikaji wa ngozi na hatua za utengenezaji wa bidhaa zake vikiwemo viatu na mikanda kutokana na ukweli kuwa Kishapu ina utajiri wa mifugo.
Utajiri huo wa mifugo pia unawezesha kiwanda kidogo cha usindikaji maziwa na utengezaji wa ‘yoghart’ ambayo katika banda hilo wananchi mbalimbali waliopita walipata elimu kutoka kwa ofisa mifugo wa wilaya, Dk. Aphonce Babyambagaki.
Sherehe za Nanenane katika kanda ya Ziwa ziliambatana na burudani mbalimbali ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiu, Anthony Mtaka.
Pia sherehe zilizojumuisha mikoa mbalimbali nchini na kitaifa zilifanyika mkoani Lindi na mgeni rasmi alikuwa ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa