Na Ofisi ya Habari, Kishapu
Halmashauri ya wilaya ya Kishapu imepongezwa kwa hatua yake ya utekelezaji miradi mbalimbali ya maendeleo kwa ufanisi pamoja na changamoto za uhaba wa fedha.
Pongezi hizo zimetolewa leo na mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Boniphace Butondo wakati akifungua kikao cha Baraza la Madiwani kilichoketi kupokea taarifa za kata kwa kipindi cha robo ya nne ya mwaka.
Butondo alisema miradi hiyo imetekelezwa kwa kiwango kizuri pamoja na changamoto ya uhaba wa fedha iliyoikabili halmashauri hiyo kwa kipindi hicho.
Alisema ushirikianoa baina ya madiwani na wataalamu kutoka halmashauri hiyo ndiyo siri ya mafanikio hayo ambayo ni tija kwa wananchi wanaowahudumia.
Aidha, aliwapongeza wataalamu hao kutoka idara mbalimbali kwa kuwa na usimamizi mzuri ikiwemo wa fedha na maeneo ambayo miradi hiyo inatekelezwa na kuwataka waendelee kushikamana.
“Naomba niwapongeze wote kwa ushirikiano mkubwa mnaounesha najua kuna changamoto ya kuwa na mapato kidogo kutokana na hali ya hewa na hivyo kuchangia kutopata pamba kwa wingi ambayo inaingiza mapato halmashauri,” alisema.
Mwenyekiti huyo ambaye pia ni diwani wa kata ya lagana aliishukuru ofisi ya mkuu wa wilaya kwa ushirikiano mkubwa kwa halmashauri na hivyo kuchangia mafanikio hayo.
Tayari miradi mbalilimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa, zahanati, barabara na maji imetekelezwa katika kata mbalimbali za halmashauri ya wilaya hiyo.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa