Na Ofisi ya Habari, Kishapu
Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga imesajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto 47,527 wenye umri wa chini ya miaka mitano tangu kampeni hiyo izinduliwe rasmi wilayani humo.
Ofisa Maendeleo ya Jamii wa wilaya hiyo, Joseph Swalala amebainisja hayo ofisini kwake wakati akitoa takwimu za kampeni ya usajili watoto wenye umri huo inayoendelea wilayani humo.
Kampeni hiyo inaratibiwa na Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi (RITA) kwa ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF) inahusisha watoto wa umri wa chini ya miaka mitano.
Swalala alisema kuwa vijiji vyote 117 vilivyopo kwenye kata zote 25 za Wilaya ya Kishapu vinafikiwa ili kutoa vyeti kwa watoto na kupata takwimu zao.
Alibainisha walikadiria kuwafikia watoto 56,235 lakini kutokana na changamoto ya vitendea kazi ikiwemo uhaba wa vitabu vya usajili ni asilimia 86 pekee ya lengo ndio iliyofikiwa hadi sasa.
Mkuu huyo wa idara hiyo alitaja changamoto nyingine kuwa ni uhaba wa magari kwa ajili ya kusambaza vitendea kazi na rasilimali watu ambapo alisema wamejitahidi kuyatumia kama yalivyo ili kazi ifanyike.
“Mwitikio wa wananchi katika kampeni hii ni mkubwa na tunaona akinamama wengi wanafika katika vituo vya uandikishaji vilivyopo kata mbalimbali katika wilaya yetu,” alisema.
Kampeni hiyo ilianza Machi 21 mwaka huu ikiwa na lengo la kutatua changamoto ya uhaba wa vyeti vya kuzaliwa kwa wananchi.
Alifafanua kuwa inakadiriwa kuwa wananchi wengi hawana vyeti vya kuzaliwa kutokana na sababu mbalimbali, hivyo kutokana na kampeni hiyo Serikali itaweza kupanga mipango yake kwa urahisi na kwa ufanisi.
RITA ilizindua mpango mkakati wa usajili wa kisasa wa watoto chini ya miaka mitano unaolenga kuongeza idadi kwa kiasi kikubwa cha usajili sanjari na kuboresha mfumo wa usajili Tanzania Bara.
Mpango Mkakati huu wa usajili umezinduliwa katika mkoa wa Mbeya ,mpango huu ni endelevu na utatekelezwa katika halmashauri zote katika mkoa wa Shinyanga na baadae utakwenda katika mikoa mingine Tanzania Bara.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa