Zoezi la kuapishwa kwa Waheshimiwa Madiwani wanao ziwakilisha kata 29 za Wilaya ya Kishapu limefanyika leo Desemba 14,2020 katika ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu likisimamiwa na Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Kishapu, Amana Ismail ambapo wameaswa kufanya kazi ya kuihifadhi, kuilinda na kitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa sheria za Tanzania.
Akizungumza wakati wa kufungua zoezi la kuapishwa madiwani hao Katibu Tawala wa Wilaya ya Kishapu, Shedrack Kengese amesema jukumu la kwanza ambalo wanatakiwa kwenda kuanza nalo ni ujenzi wa shule, vyumba vya madarasa pamoja na madawati ili wanafunzi watakaoanza masomo Januari mwaka 2021 wasome kwenye mazingira rafiki.
“Mmechukua jukumu la kuwatumikia wananchi hivyo nawaomba mkatatue changamoto zote zinanowakabili wananchi, hata kama jambo liko nje ya uwezo wako peleka ngazi za juu. Shirikianeni na wananchi hasa katika hili la ujenzi wa Vyumba vya madarasa pamoja na madawati ili wanafunzi wasikae chini ya miti” alisema Kengese.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Taraba wakati akitoa salamu kwenye zoezi hilo la uapisho amesema wilayani humo kutakuwa na idadi kubwa ya wanafunzi waliofaulu kuingia kidato cha kwanza hivyo kuna baadhi ya kata zinatakiwa kujengwa shule mpya.
Akitaja kata hizo kuwa ni Lagana, Sekebugoro, Isoso, Mwaweja, Shagihilu, Mwasubi na Bupigi na kuwataka Madiwani hao kufanya kazi hiyo ya ujenzi wa shule mpya pamoja na ujenzi wa vyumba vya madarasa na madawati kwa kushirikiana na wananchi kuchangia shughuli hizo za maendeleo.
Nao baadhi ya madiwani hao akiwemo Mheshimiwa Edward Nkuba kutoka Kata ya Kiloleli amesema watakwenda kulifanyia kazi swala hilo la upungufu wa vyumba vya madarasa, madawati na ujenzi wa shule kwa kushirikiana na nguvu a wananchi pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo kama vile Mdogi wa Almasi wa Williamson.
Naye mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Ndugu, Emmanuel Johnson aliwaomba Waheshimiwa Madiwani kuwa na ushirikiano wa kutosha kwenye ujenzi wa miundombinu hizo za ujenzi wa vyumba vya madarasa kwani tayari wameshaanza ujenzi wa vyumba vya madarasa kwenye baadhi ya kata.
Kwa upande wa mbunge wa Jimbo la Kishapu, Mheshimiwa Boniphace Butondo aliahidi kushirikiana vyema na madiwani hao ambapo ifikapo Januari mwaka 2021 ataanza ziara za kukagua miradi ya maendeleo huku akiwataka kukamilisha na kuanzisha miradi mipya iliyoibuliwa kulingana na mpango wa bajeti hasa ujenzi wa madarasa ili wanafunzi wasome kwenye mazingira rafiki. Aidha Mbunge huyo aliwaasa madiwani kufanya kazi kulingana na Ilani ya Chama cha Mapinduzi huku wakiipinga rushwa.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa