Watanzania wametakiwa kutambua umuhimu wa kupima afya zao na kuchukua hatua mapema ikiwa ni pamoja na kujikinga na maambukizi mapya ya Virusi Vya UKIMWI kwa kuwa waaminifu na kuzingatia matumizi sahihi ya kondomu wakati wa tendo la ndoa.
Rai hio imetolewa leo Desemba 1,2019 na mkuu wa wilaya ya Kishapu mkoa wa Shinyanga Bi.Nyabaganga Taraba wakati wa maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani yaliyofanyika kimkoa katika kijiji cha Negezi kata ya Ukenyenge wilayani Kishapu.
Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga Bi.Zainab Terack, mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa UKIMWI upo na bado hauna chanjo wala tiba, hivyo ni vyema wananchi wakajitokeza kupima afya zao na kuchukua hatua za mabadiliko ya tabia.
"Naomba tuachane na mila potofu zinazochochea maambukizi mapya ya Virusi Vya UKIMWI, wanaume jitokezeni kupata huduma ya tohara kinga, ili kupunguza kasi ya maambukizi pia tuimarishe ulinzi wa watoto kwa kuwapa elimu mapema juu ya mimba na ndoa za utotoni kwa kukemea mila kandamizi ambazo ni mojawapo ya chanzo cha maambukizi mapya ya Virusi Vya UKIMWI kwa watoto wetu"amesema Taraba.
Naye mratibu wa kuthibiti UKIMWI kwa mkoa wa Shinyanga, Dr, Peter Mlacha wakati akitoa taarifa ya VVU/UKIMWI kimkoa amesema kuwa, kutokana na mkoa kuwa na ushamiri mkubwa wa maambukizi ya UKIMWI, mkoa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo tunaendelea kupambana na kuthibiti maambukizi mapya ya VVU, kwa kutoa huduma na elimu kwa wananchi juu ya VVU/UKIMWI. Huduma kama vile, upimaji wa maambukizi ya UKIMWI, matunzo na tiba, huduma ya kuzuia maambukizi kutoka kwa mama mjamzito kwenda kwa mtoto, huduma za tohara kwa wanaume, huduma za magonjwa ya ngono na via vya uzazi, huduma za wagonjwa majumbani, UKIMWI mahala pa kazi, huduma kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia na ukatili Dhidi ya watoto nk.
Aidha katika kutekeleza mkakati wa 90, 90, 90, serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imejipanga kuhakikisha kuwa 90% ya watu wanaoishi na VVU wanatambua hali zao za maambukizi, 90% ya watu wenye maambukizi wanatumia dawa za kufubaza VVU na 90% ya watu wanaotumia dawa za kufubaza VVU wanakuwa na idadi ya VVU kwa kiwango kidogo kabisa mwilini, huku kauli mbui ya maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani mwaka 2019 ikiwa ni "jamii ni chachu ya mabadiliko, tuungane kupunguza maambukizi mapya ya Virusi Vya UKIMWI".
Miongoni mwa wadau walioshiriki kufanikisha maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani na pamoja na AGPAHI, CUAMM, JHPIEGO, Tanzania Redcross, Intrahealth International, THPS, Thubutu Africa Initiatives, USAIDS, Tulonge Afya na DSW.
Na Catherine J. Ngowi
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa