Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa amesema Serikali imetoa sh. milioni 534 kwa ajili ya kuboresha miundombinu katika shule za msingi na sekondari Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu.
Amesema pia imetenga sh. milioni 81 itakazotoa kwa ajili ya ujenzi wa maabara kwenye shule za sekondari zilizopo wilayani humo ili wanafunzi waweze kufanya majaribio ya sayansi.
Mhe. Majaliwa amesema hayo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Mwangongo wilayani humo alipofanya ziara ya kikazi kutembelea miradi ya maendeleo na kuzungumza na watumishi na wananchi.
Alisema katika fedha hizo jumla ya sh. milioni 223 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa kwenye shule za msingi katika Halmashauri ya wilaya hiyo ili kuwawezeha watoto wawe na mazingira mazuri ya kusoma.
Mhe. Waziri Mkuu aliongeza kuwa Serikali imetoa sh. milioni 81 kwa ajili ya kuongeza vyumba vya madarasa katika shule za sekondari yakiwemo ya wanafunzi wa kidato cha tano na sita.
Aidha, alisema Serikali imetoa sh. milioni 230 kwa ajili ya kuongeza mabweni na vyumba vya madarasa katika Shule ya Sekondari Shinyanga wilayani Kishapu ili wanafunzi waweze kupata nafasi ya kulala.
“Natoa mwito kwenu wananchi kila kijiji chenye shule ya msingi kianze kutathmini ni watoto wangapi wataanza shule mwezi wa kumi na mbili ili kuanzia mwezi wa nane waanze kuongeza vyumba vya madarasa na kila kata fanyeni tathmini kubaini ni wanafunzi wangapi wataingia sekondari ili muongeze vyumba vya madarasa kama havitoshi,” alisema.
Aliahidi kuwa Serikali itatoa sh. milioni 81 kwa ajili ya ujenzi wa maabara zingine katika shule za sekondari wilayani humo na kuwa zikikamilika itapeleka vifaa vya majaribio.
Alisema malengo ya Serikali ni kukamilisha ahadi zote alizotoa Mheshimiwa Rais na kuwa zitakamilishwa kwa zaidi ya asilimia 90 hivyo wananchi waendelee kuiamini Serikali.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa