Baraza la Madiwani wamefanya kikao cha kujadili majibu ya hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali za mwaka 2018/2019 leo tarehe 03 June 2020 tika ukumbi wa Soko la wajasiriamali Kishapu ambapo kikao hicho kimeongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mh. Boniphace Butondo ambaye pia ni Diwani wa kata ya Lagana.
Katika kikao hicho Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya ya Kishapu Sostenes Mbwilo aliwasilisha majibu ya hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu za Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kwa mwaka ulioisha tarehe 30/06/2019 ambapo Halmashauri ya Kishapu ilikuwa na jumla ya hoja 84 kati ya hizo, hoja 33 ambapo ni sawa na asilimia 39% zimetekelezwa kikamilifu na hoja 40 ambazo ni sawa na asilimia 48% ziko katika utekelezaji na majibu yake yamewasilishwa ofisi ya ukaguzi Shinyanga zikisubiri uhakiki, hoja 4 ambapo ni sawa na asilimia 5% zimepitiwa na hoja 7 ambapo ni sawa na asilimia 8% zimerudishwa kwa kuwa zinahitaji majibu ya nyongeza hivyo zinasubiri uhakiki katika ofisi ya ukaguzi Shinyanga.
Aidha, naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Albert G. Msovela ameipongeza Halmashauri kwa kupata hati safi kwa utendaji bora wa kazi huku akishauri kitengo cha manunuzi kuhakikisha wanafanya manunuzi kwa kushindanisha ubora na bei ya bidhaa na kuyafanya ndani ya mfumo wa manunuzi wa Halmashauri
“Halmashauri imeendelea kupata hati isiyokuwa na mashaka hivyo tuendelee kufanya vizuri, manunuzi yote katika kitengo cha manunuzi yafanyike ndani ya mfumo wa halmashauri ili kuepuka hizi hoja, hivyo mhakikishe mapungufu haya hayajitokezi ili Halmashauri iendelee kupata Safi” alisema Msovela.
Kadhalika, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Zainab Telack ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kwa kutekeleza miradi mingi ya maendeleo na kazi nyingine pia za Halmashauri zimefanyika kwa kiwango kinachotakiwa kama miradi ya vituo vya afya Songwa na Kishapu.
“tuna miradi mingi ambayo tumeitekeleza kama mkoa na kama Halmashauri ya Kishapu, na kazi nyingi tulizopangiwa kuzifanya zimafanyika kwa kiwango kinachotakiwa na ndani ya muda ambao tulipewa kufanya, hii ni kutokana na ushirikiano baina ya madiwani na wataalamu” alipongeza Terack
Vile vile, Mkuu wa Mkoa aliwashauri madiwani kukuepuka kufanya kampeni kabla ya muda uliopangwa na serikali wa kufanya kampeni bila kusahau kushauri wananchi wanaofanya biashara ndogondogo kununua vitambulisho vya ujasiriamali kuepuka kulipa kodi iliyo nje ya uwezo bila kusahau kuwashauri kuhifadhi mazao ya chakula kwa ajili ya matumizi ya baadaye.
“naombeni madiwani muache kutumia fedha tunapoelekeza kwenye uchaguzi kuweni makini. Kama umefanya kazi nzuri wananchi ndio wataamua kutokana na ulivyopanda ” alisemaTelack
“ Watu waache kuuzia mazao shambani, endeeni kuwapa elimu wananchi na kila mtu ahakikishe ana chakula cha mwaka huu na mwaka kesho. Tumeshasema hadi kwenye vyombo vya habari kuwa watu waache kuuza chakula na wale ambao hawakupata mazao wanunue sasa bei ya mazao ikiwa bado chini” aliongeza.
“corona ipo tuchukue tahadhari”
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa