Maafisa ugani halmashauri ya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga wameagizwa kusimamia kikamilifu sheria ndogo inayotaka kila kaya kulima mazao yanayostahimili ukame.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa wilaya hiyo, Nyabaganga Taraba wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kuhamasisha shughuli za kilimo kijiji cha Malwilo wilayani hapa juzi.
Akizungumza kwa niaba ya mkuu huyo, Katibu Tawala wa Wilaya, Shadrack Kengese alisema Kishapu hupata mvua chini ya wastani hivyo mazao huathiriwa na ukame.
Alisema kwa kutambua hali ya hewa halmashauri ilitunga sheria ndogo mwaka 2008 ya kilimo cha mazao yanayostahimili ukame na hifadhi ya chakula cha kutosha kwa kila kaya.
“Maofisa ugani wasimamie kikamilifu utekelezaji wa sheria hii na yeyote anayekaidi afikishwe kwenye vyombo vya sheria. Adhabu yake ni kifungo kisichozi miezi kumi na miwili, kulipa faini shulingi laki tatu au vyote,” alisema.
Kengese alifafanua kuwa kampeni hiyo ambayo kimkoa ilizinduliwa Agosti mosi inashirikisha wananchi katika vijiji vyote vya wilaya ili kuinua hali za wananchi kiuchumi na kielimu.
Aidha, katibu tawala huyo aliongeza kwa kuwataka wananchi kutumia vizuri fursa ya ardhi iliyopo wilayani Kishapu kwa kujiletea maendeleo kupitia shughuli za kilimo.
Kwa upande wake Afisa Kilimo wilayani humo, Godwin Everygist aliwatahadharisha wananchi kutokuuza chakula na kuwa na akiba kwa ajili a matumizi panapokuwa na changamoto ya upungufu.
Aliwataka wananchi waanze kuandaa mashamba yao maema kutokana na taarifa ya kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) kuonesha mvua kuwahi kunyesha.
Alisema Serikali inatarajia kuanza kusambaza pembejeo za pamba kwa wakulima hivyo waanze kutumia wakati huo kufanya maandailizi ya mashamba mapema.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa