Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainabu Terack amefanya ziara leo tarehe 23 March 2020 ya kukagua hatua za mwisho za maandalizi na ujenzi katika eneo la makinikia Mwadui wilayani Kishapu.
Katika ziara hio alionyesha kuridhika na maandalizi hayo huku akitoa angalizo juu ya ugonjwa wa COVID-19 ambapo aliutaka uongozi wa eneo hilo pamoja na Halmashauri kuchukua tahadhari mapema kwa kuweka mazingira safi na rafiki kwa kuweka maji safi tiririka na sabuni ya maji katika mageti yote huku akisisitiza kutumia kifaa cha kupima hali joto aina ya ‘thermo Scanner’ ili kumpima kila anayeingia ndani ya eneo hilo.
“Naomba tuwe makini sana, hakuna anayetaka kuja hapa aondoke na huu ugonjwa tumekuja kutafuta tusitafute ugonjwa, tuweke mazingira kuwa rafiki kwa watu kwa kuweka maji safi tiririka, sabuni ya maji na sanitizers, muweke ndoo za maji kwenye kila banda. Hakuna sababu ya kuleta watoto hapa, na yoyote ambaye hana sababu maalumu ya kuzurura akae nyumbani. Hakuna aliyeko salama kati yetu, tukilijua hilo kila mtu atajikinga, likiingia haliangalii cheo wala rangi, tumejifunza kwa wenzetu, wao walichelewa kujikinga, sisi tumewahi. Ikifikia hali ya kujitibu wa kukutibu hayupo anaumwa yuko kwenye karantini, hivyo tuchukue tahadhari.” Alisema Terack.
Katika eneo hilo la ‘kuchenjulia’ almasi inatarajiwa kuanza kazi rasmi tarehe 25 March 2020 ambapo kwa kila siku vitaingia vikundi 100 ambapo kikundi kimoja kina watu 10 hivyo idadi ya watu kuwa 1,000. Katika eneo hilo kutakuwa na huduma ya mama lishe, walinzi, na wahudumu wengine hivyo kufanya jumla kuu waka na idadi ya watu zaidi ya 3,000 kila siku.
Kwa Tanzania hadi sasa kuna jumla idadi ya wagonjwa wa Corona 12 ambapo nane kati yao ni raia wa Tanzania na wengine wanne ni raia wa kigeni. Ugonjwa huu kwa Tanzania haujaripotiwa kuua mtu hata mmoja. Katika juhudi za kudhibiti kuenea kwa maambukizi wageni wote wanaoingia nchini kutoka katika mataifa yaliyoripotiwa kuwa na ugonjwa huo watatengwa kwa siku 14. Aidha agizo hilo lililotolewa na Raisi wa Jamuhuri wa Muungano wa Tanzania,John Pombe Magufuli linawajumuisha Watanzania wanaorejea nyumbani kutoka nchi nyingine.
Hatua nyingine zilizochukuliwa kuthibiti ugonjwa huu ni pamoja na kufunga shule zote kwa muda wa siku 30 pamoja na kuzuia mikusanyiko yote ya watu wengi yakiwemo matamasha ya mziki,mikutano ya hadhara mbalimbali ikiwemo ya kisiasa.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa