Katika harakati za kusukuma gurudumu la maendeleo ya kielimu nchini Tanzania, Mwakasege Foundation imetoa msaada wa madawati 200 katika shule ya msingi Bubiki B iliyopo katika wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga. Madawati hayo yenye thamani ya shilingi milioni 14 yametolewa rarehe 15/01/2020 na Mchungaji Christopher Mwakasege katika shule hio. Katika makabidhiano hayo Mchungaji Mwakasege aliushukuru uongozi wa shule kwa kukubali kupokea msaada huo ikiwa ni harakati za kuchangia maendeleo ya kielimu vijijini.
“Mwakasege foundation inaushukuru uongozi wa shule ya msingi Bubiki B kwa kukubali kuupokea msaada huo kidogo. Madawati haya yatapunguza adha ya wanafunzi waliokuwa wanakaa chini waweze kusoma katika mazingira rafiki kielimu, tunazidi kumshukuru Mungu kwa kuwa madawati yote yamefika kama tulivyokusudia”.
Mchungaji Mwakasege pia alitoa rai kwa wanafunzi pamoja na uongozi wa shule hio kutunza vizuri madawati hayo ili yatumike kwa muda mrefu yakisaidia na wengine kwa baadae. Aidha alisema watakaa na kamati yake kuona watakachoweza kukifanya kutokana na uhitaji wa shule hiyo na wilaya kwa ujumla.
Kadhalika mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu, Stephen Ndaki wakati akipokea madawati hayo alishukuru kwa msaada huo huku akiwataka wanafunzi kuyatunza na kusoma kwa bidii.
Naye mwalimu mkuu wa shule ya msingi Bubiki B, Venosa Msafi katika hafla hiyo ya kukabidhiwa madawati alitoa pongezi na shukrani kwa uongozi wa Mwakasege Foundation kwa msaada huo kwani itapunguza changamoto ya watoto kukaa chini, huku akiahidi ufaulu mzuri kwa wanafunzi wake kwani watasoma kwenye mazingira rafiki ya elimu bora. Shule hiyo pia inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa matundu ya vyoo na vyumba vya madarasa.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa