Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Zainab Telack amezipongeza shule zilizofanya vizuri katika mitihani ya sekondari na msingi iliyofanyika mwaka 2018 Wilaya ya Kishapu.
Pamoja na pongezi hizo ameagiza kila shule kuhakikisha zinajenga vyumba viwili vya madarasa ili kuhimili idadi kubwa ya wanafunzi wanaojiunga na shule mwaka ujao.
Pongezi na maagizo hayo vimetolewa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Nyabaganga Taraba Februari 21, 2018 wakati wa kikao cha tathmini ya matokeo hayo ya mitihani.
Mhe. Telack aliagiza kuwepo kwa mpango wa kuwashirikisha wazazi na wananchi kwa ujumla kuhakikisha kila inatoa chakula cha mchana kwa wanafunzi wake hatua itakayochangia uboreshaji wa elimu.
Alisema kwa mwaka huu wilaya hiyo haina upungufu wa vyumba vya madarasa na hivyo shule zijipange kupokea wanafunzi wengi zaidi mwaka ujao kwa kujenga madarasa.
Katika hotuba hiyo alisisitiza mazoezi ya mara kwa mara kwa wanafunzi wote na kuzitaka shule ziweke utaratibu wa kuwapa majaribio ya wiki ili kuwajengea morali wa kujisomea.
Aidha, Mkuu huyo wa mkoa aliagiza zianzishwe klabu za masomo mbalimbali na kuzishindanisha jambo litakalosaidia kuinua kiwango cha elimu kwa kiwango fulani.
Kwa upande mwingine aliwapa angalizo wazazi kuhakikisha watoto wao wanakwenda shule huku akikemea ‘biashara’ ya mimba vitu ambavyo vinaporomosha kiwango cha elimu.
Kikao hicho kilifuatiwa na hafla ya kuzipongeza shule zilizofanya vizuri zaidi kiwilaya zikiwemo Shule ya Msingi Shagihilu na Shinyanga Sekondari ‘Shy Bush’.
Hafla hiyo pia ilienda sambamba na tukio la kumuaga Ofisa Elimu wa Vifaa na Takwimu, Richard Mutatina aliyehamishiwa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.
Kwa umoja wao walimu pamoja na maafisa Elimu kata walimpa pongezi na kumshukuru kwa utumishi wake akiwa Kishapu.
Pia walimpa zawadi mbalimbali ikiwa ni ishara ya kumuonesha upendo kama ambavyo waliishi nae kipindi chote akitumia Idara hiyo.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa