Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Zainab Telack amewataka wananchi kutunza vyanzo vya maji katika maeneo yao ili yaweze kuwasaidia katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
Mhe. Telack amesema hayo leo wakati alipofanya ziara ya kikazi wilayani Kishapu kwa ajili ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa.
Alipiga marufuku wananchi kufanya shughuli za kibinadamu kando kando ya vyanzo hivyo vya maji zikiwemo kilimo cha mbogamboga isipokuwa tu umbali unaotakiwa wa kuanzia mita 60 kutoka kwenye chanzo.
“Tutunze vyanzo vya maji ili vitutunze si mnaona mnaweza kufanya shughuli za ujenzi kwa kutumia vyanzo hivi vya maji sasa kama mngeviharibu mngelazimika kununua maji kwa ajili ya ujenzi.
Mhe. Mkuu wa Mkoa akiwa na Kamati za Ulinzi za Wilaya na Mkoa alikagua ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Unyanyembe unaofadhiliwa na Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
Mradi huo wenye thamani ya jumla ya sh. milioni 453 ambao chanzo chake ni maji ya Ziwa Victoria unatarajiwa kuwa mkombozi kwa wananchi wa kijiji hicho pamoja na vijiji vya jirani.
Kwa upande wake Mhandisi wa Maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Lucas Said alisema kuwa mradi huo ulianza Novemba mwaka jana na unatarajiwa kukamilika Aprili mwaka huu.
Wananchi katika baadhi ya vijiji vya kata ya Uchunga ambapo mradi huo unapita kupitia kwa wenyeviti wao, Samson Daudi na Dominico Chipa waliipongeza Serikali kwa kuwakumbuka.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa