Asasi isiyo ya kiserikali ya Msaada na Mandeleo ya Jamii (REDESO) imetoa mafunzo ya urasimishaji na mpango wa biashara kwa wakulima na wasindikaji mkonge kutoka wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga na Meatu mkoani Simiyu.
Mafunzo hayo yaliyofanyika wilayani hapa kwa ushirikiano pia na Shirika lisilo la kiserikali la OXFAM yalilenga kuwajengea wakulima hao uwezo na mbinu za kuongeza faida.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Meneja Mradi wa REDESO Wilaya ya Kishapu, Charles Buregeya alisema washiriki wanawezeshwa kupata mbinu za kuandaa mpango kazi na kusajili biashara zao.
Alisema wengi wa wakulima na wasindikaji wa zao hilo linalofanya vizuri katika wilaya hizo wanakosa mbinu za biashara hivyo kupitia mafunzo watakuwa na uwezo wa kutafuta masoko.
Buregeya aliongeza kuwa ili waweze kuwa na uwezo wa kutafuta masoko mafunzo hayo yanajumuisha pia kupatiwa mbinu za ushawishi na kuweza kuuza bidhaa zao na kupata faida.
Alisema pia mafunzo hayo yaliyotolewa na mwezeshaji kutoka asasi isiyo ya kiserikali ya Feasible Resource, Yared Babona yanalenga kuwawezesha washiriki kulifanya zao hilo kuwa na tija na manufaa zaidi.
Redeso inafanya kazi na mamlaka za Serikali za Mitaa katika halmashauri hizo mbili za wilaya kwa kuendesha mafunzo hayo kwa wilaya hizo mbili kupitia wanachama wa Shirikisho la Wasindikaji Meatu na Kishapu (SHIWAMKI).
“Ukweli ni kuwa shirikisho hili bado ni changa lakini kutokana na mazungumzo tuliyofanya na Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB) lina uwezo wa kufanya vizuri katika ukanda huu wa Ziwa Victoria endapo hatua za haraka zikichukuliwa,” alisema.
Hivyo, alisema ili hayo yote yaweze kufanikiwa taasisi hiyo imekuwa ikitoa mafunzo kwa makundi ya wakulima na wasindikaji wa zao hilo ambalo limekuwa likifanya vizri katika ukanda huo.
Mkonge ni mojawapo ya mazao yaliyoonesha mafanikio makubwa katika Wilaya ya Kishapu kutokana na kuhimili hali ya ukame ambayo huwa ni changamoto kubwa kutokana na uhaba wa mvua.
Hivyo halmashauri ya wilaya hiyo inachukua hatua mahsusi za kuhamasisha kilimo hicho kwa kuwa kimeonesha tija kubwa hivyo kinaweza kuleta maendeleo makubwa katika sekta ya kilimo.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa