Serikali mkoani Shinyanga kwa kushirikiana na mashirika mablimbali yasiyo ya kiserikali yanayojishughulisha na utekelezaji wa miradi ya utetezi wa haki za wanawake na watoto mkoani Shinyanga, wameadhimisha siku ya wanawake duniani.
Maadhimisho hayo yamefanyika leo Machi 8, 2021 katika kijiji cha Kangeme Kata ya Ulowa Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama, na kuhudhuliwa na wadau wa maendeleo kutoka mashirika mbalimbali, watumishi wa Serikali, pamoja na wananchi, ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mheshimiwa Zainab Telack.
Akizungumza kwenye maadhimisho hayo, Telack amewataka wanawake mkoani Shinyanga kujituma kufanya kazi kwa bidii, pamoja na kujiunga kwenye vikundi vya ujasiriamali, na kupata mitaji ya kuanzisha biashara mbalimbali kupitia fedha za Halmashauri asilimia 10, ili wajikwamue kiuchumi na kuacha kuwa tegemezi kwa waume zao.
Amesema mwanamke ni nguzo katika familia, ambapo akitetereka familia inayumba ikiwa ni pamoja na watoto kuishi mazingira magumu, na hivyo kuwataka waache kubweteka bali wajitume kufanya kazi bila kukata tamaa, huku wakishirikiana na waume zao kufanya maendeleo.
“Licha ya baba kuwa ndio kichwa cha familia, lakini mwanamke yeye ni nguzo katika familia kwa sababu hawezi kutelekeza watoto wake kama wanavyofanya wanaume kutokana na kujua uchungu wa kuzaa, hivyo mkiwa imara kiuchumi maisha yenu yatakuwa mazuri sana pamoja na kujawa na amani,”amesema Telack.
“Fedha zipo za mikopo bila riba kwenye Halmashauri, hivyo jiungeni kwenye vikundi vya ujasiriamali, ili mpate kukopesheka na kupata fedha za mitaji na kuanzisha biashara mbalimbali na kujikwamua kiuchumi, hii itawasaidia kuacha kuwa tegemezi kwa waume zenu bali mjisimamie nyie wenyewe,”ameongeza Telack.
Katika hatua nyingine alikemea vitendo vya wananchi kuendekeza mila na desturi kandamizi, ambazo zimeendelea kuwa chanzo cha kuwepo kwa matukio ya ukatili wa kijinsia, vikiwamo vipigo kwa wanawake, kukatisha ndoto za watoto wa kike kwa kuwaozesha ndoa za utotoni, na kuonya kuwa Serikali itaendelea kuwachukulia hatua watu wa namna hiyo.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga Albert Msovela, akisoma taarifa ya mkoa kwenye maadhimisho hayo ya wanawake duniani mkoani Shinyanga, ametaja takwimu za matukio ya ukatili wa kijinsia, kuwa kuanzia kipindi cha Julai 2019 hadi Desemba 2020 yamepungua kulinganisha na miaka ya nyuma, na kubainisha kuwa Serikali inaendelea kutatua changamoto za matukio ya ukatili, kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali mkoani humo ili jamii iendelee kuwa salama.
Nao baadhi ya wanawake ambao walihudhuria kwenye maadhimisho hao akiwemo Ester John kutoka kijiji cha Kangeme Kata ya Ulowa- Ushetu, alipongeza Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya ya kutokomeza matukio hayo ya ukatili wa kijinsia, na kuomba elimu izidi kutolewa zaidi hasa maeneo ya vijijini ambapo bado kuna ukatili.
Aidha mashirika ambayo yameshiriki kwenye maadhimisho hayo ni Relief For Development Society (REDESO), Thubutu, Africa Initiative, Agape, Investing in Children and Their Society (ICS), Shidepha, Rafiki SDO, PACESH, HUHESO Foundation, Msichana Initiative, pamoja na kampuni ya vinywaji ya Jambo (Jambo Food Products).
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa