Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Terack leo tarehe 2 June 2020 amefanya ziara katika shule ya Sekondari Shinyanga na shule ya Sekondari Kishapu zenye wanafunzi wa kidato cha tano na sita kukagua hali ya maandalizi kwa shule hizo dhidi ya Corona. Hali hiyo imetokana na agizo la Mheshimiwa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli la kuwataka wanafunzi hao kurudi shule baada ya shule zote kufungwa kwa dharura kutoka mwezi Machi kwa ajili ya janga la corona.
Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa ameutaka uongozi wa shule hizo kufundisha wanafunzi njia bora za kujikinga dhidi ya ugonjwa wa corona kama vile kunawa mikono kwa usahihi huku wakihakikisha kuna vifaaa muhimu kwa ajili ya kujikinga na corona kama vile ndoo za kunawa mikono na sabuni za maji na barakoa.
“Nia yetu ni kuhakikisha kuwa mnakuwa salama, wanafunzi wakipata maambukizi na nyie walimu mtapata, jikingeni kwa sababu corona ipo. Pia katika mabweni yao ya kulala hakikisheni wanapata nafasi za kutosha wasibanane. Nanyi Maafisa elimu shirikianeni na walimu katika kipindi hiki cha corona mkitatua changamoto katika shule hizi” alisema Terack.
Aidha Mkuu wa Mkoa amewataka wanafunzi kusoma kwa bidii kwa kushirikiana pamoja ili kujiandaa vyema na mitihani ijayo. Pia ameutaka uongozi wa shule kuhakikisha wanafunzi wanakula chakula bora na kwa wakati ili kufanya vyema katika masomo yao.
“Someni kwa pamoja kwa sababu tunataka wote mtoke mkiwa mmefaulu hivyo mshirikiane na msaidiane kwenye masomo angalau kila mtu aweze kufaulu kwenda chuo kikuu. Sasa hivi acheni kulala, tumieni huu muda uliobaki vizuri kwa sababu hatutaki ‘divisheni three wala sifuri’ nataka kuona kila mtu akipata ‘divisheni one’ nanyi walimu wasaidieni hawa wanafunzi nataka ‘divisheni one na two’ kwenye huu mkoa” aliongeza Mkuu wa Mkoa.
Kulingana na ratiba iliyotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia chini ya Waziri mwenye dhamana Profesa Joyce Ndalichako, wanafunzi wa kidato cha sita wanatarajia kuanza mtihami wa Taifa tarehe 29 June 2020.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa