Shirika la TCRS (Tanganyika Christian Refugee) wametoa taarifa ya Upembuzi ya Ufuatiliaji Rasilimali za Umma (PETS) katika sekta ya Maji wilayani Kishapu leo tarehe 25 Februari 2021 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu wakiwemo wajumbe wa kamati za PETS ngazi ya Kijiji, Madiwani, pamoja na KASHWASA wakiongozwa na Kwenyekiti wa kikao hicho Mhe. Mkuu wa wilaya ya Kishapu Nyabaganga Taraba.
Taarifa hiyo ya Ufuatiliaji wa Rasilimali za Umma inatimiza matakwa ya kikatiba katika ibara ya 27 (1) na (2) isemayo “kila mtu ana wajibu wa kulinda mali asilia ya Jamhuri ya Muungano, mali ya mamlaka ya nchi, na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi , na pia kuiheshimu mali ya mtu mwinne” na pia ibara ndogo ya pili “watu wote watatakiwa kutunza vizuri mali ya mamlaka ya nchi na ya pamoja, kupiga vita aina zote za ubadhirifu, na kuendesha uchumi wa Taifa kwa makini kama watu ambao ndio waamuzi wa hali ya baadae ya nchi.
PETS imelenga kuwasilisha taarifa ya hali halisi ya utekelezaji wa miradi ya maji inayolenga kuboresha huduma ya maji safi na salama katika vijiji kumi katika wilaya ya Kishapu vikiwemo kijiji cha Ikonongo, Ndoleleji, Maganzo, Mwamadulu, Masagala, shagihilu, Ukenyenge, Bunambiyu, Bubiki na Bubiki B ambako kuna miradi inayofadhiliwa na serikali pamoja na wadau wengine wa maendeleo ikiwemo michango ya nguvu za wanananchi.
Wajumbe wa kamati hizo wamekubaliana kuwa jamii ipate elimu ya kutosha kuhusiana na utunzaji wa vyanzo vya majo pamoja ushiriki wa nguvu kazi katika miradi ya maendeleo, kusoma taarifa za mapato na matumizi kila baada ya robo ya mwaka ili kujenga imani kwa wananchi, KASHWASA wametakiwa kutoa taarifa kwa wananchi kunapotokea itilafu ya bomba.
Akizungumza kwenye kikao hicho Mkuu wa Wilaya ya Kishapu amewataka KASHWASA kuendelea kutoa huduma bora kwa jamii na kuziba bomba zilizopasuka ili kuepuka kupoteza mapato ya nchi.
Aidha taarifa imelenga kutoa mchango stahiki katika kukuza masuala ya uwajibikaji na uwazi katika mipango, bajeti na matumizi ya fedha ya serikali na kumwezesha mwananchi kushiriki kikamilifu katika matumizi sahihi ya rasilimali za nchi kwa manufaa ya jamii kwa ujumla.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa