Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu inatarajia kupokea jumla ya sh. milioni 321 kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa ajili kujenga na kukamilisha miundombinu ya shule za msingi.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Stephen Magoiga amesema fedha hizo zitatumika katika ujenzi wa vyumba vya madarasa, vyoo na nyumba za walimu katika mwaka wa fedha 2017/2018.
Alitaja shule zitakazonufaika na fedha hizo ni Migunga iliyopo katika kata ya Mwataga ambayo imetengewa jumla ya sh. milioni 60 kwa ajili ya vyumba vitatu vya madarasa ambapo kati hizo sh. milioni 30 zimepokelewa.
Alisema tayari ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa pamoja na kingine cha ziada ambapo kwa kushirikisha nguvu za wananchi umeanza hivyo kufanya jumla yake kuwa vinne.
“Pamoja na kuwa tumepewa fedha hizo kujenga madarasa matatu lakini sisi tunafanya zaidi ya kile tulichopewa na watakagua kama tumefanya vizuri ndani ya miezi mitatu na tutapewa zawadi hivyo tunaendelea kuhamasisha jamii kushiriki katika kukamilisha miradi hii,” alisema.
Magoiga alisema kuwa mbali ya madarasa katika shule hiyo pia wanajenga nyumba moja ya walimu ya familia mbili (2 in one) ambayo itasaidia kuwapa walimu makazi karibu na shuleni hapo.
Aliongeza kuwa pia sh. milioni 30 kati ya milioni 60 zingine kutoka TEA zimepokelewa kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa na nyumba ya walimu katika shule ya msingi Idukilo katika kata ya Idukilo.
Nako halmashauri inashirikisha nguvu za wananchi katika kusimamia na kukamilisha miundombinu hiyo ya shule ambayo itasaidia kuweka mazingira mazuri ya elimu ya msingi.
Alibainisha katika shule ya msingi Maganzo kata ya Maganzo mradi ujenzi wa choo umeanza na unatarajia kugharimu sh. milioni 50 zilizotengwa na mamlaka hiyo ambapo tayari halmashauri imepokea sh. milioni 25.
Magoiga aliongeza kuwa shule ya msingi Maganzo itapokea jumla ya sh. milioni 141 kutoka TEA ambazo zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa nyumba sita za walimu.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa