Shirika la Oxfam kwa kushirikiana na Redeso wamefanya ziara wilayani Kishapu kutembelea miradi ya biashara ya vikundi katika kata ya Shagihilu,Kishapu , Lagana na Inolelo. Ziara hio ya siku mbili ilifanyika kuanzia tarehe 22 June hadi tarehe 23 June 2020 ililenga kufanya tathimini kwa kila kikundi na kuona mafanikio na mapungufu ya biashara zao na kuweka mikakati na maazimio ya pamoja kwa maendeleo ya vikundi hivyo.
Shirika la Redeso (Relief for Development Societies) linalojihusisha na usimamizi wa mazingira, uhifadhi wa vyanzo vya maji na ufumbuzi wa nishati, Ulinzi wa watoto, wanawake na uwezeshaji vijana, kupunguza athari kwa maafa Wilayani Kishapu. Swala la uwezeshaji kwa wanawake na vijana, Oxfam na Redeso wamewawezesha katika kuanzisha na kuendeleza jumla ya vitalu nyumba saba.
Vikundi hivyo vinavyojihusisha na biashara ya nyanya vimepata mafanikio makubwa kwani elimu waliyoipata imewasaidia kuzalisha na kuuza nyanya ambapo zimesaidia vikundi kukopeshana nakurudisha kwa riba hivyo kuongeza pato la kikundi. Pia kila mwanachama amefanikiwa kuanzisha kitalu nyumba kinachoongeza pato la mtu mmoja mmoja. Aidha fedha zilizotokana na biashara hiyo ya nyanya zimewasaidia wanavikundi kuongeza pato la familia na kujikwamua na umasikini.
Vikundi hivyo ni pamoja na kikundi cha Azimio Vijana kilichopo katika kata ya Shagihilu. Kikundi kina wanachama 13 kilichopo chini ya mwenyekiti Thomas Nangi. Kikundi cha Tumaini kilichopo katika kata ya Lagana kikiongozwa na Butene Mwandu. Aidha Redeso na Oxfam wamatembelea kikundi kinachoitwa Imponya Matembe kinachomiliki Solar dryer kilichopo katika kata ya Inolelo chenye wanachama 19 Soar Dryer hio ni kwa ajili ya kukaushia mboga mboga na viazi lishe, lengo ni kuhakikisha chakula kinakaushwa na kuhifadhiwa kikiwa kinabaki katika ubora wake bila kupoteza virutubisho. Kadhalika Presser iliyopo katika kata ya Igaga ikiwa katika hatua za mwisho za matengenezo, kwa ajili ya kushindilia Katani ili kusafirisha mzigo mkubwa kwa wakati mmoja hivyo kurahisisha usafirishaji wa malighafi hiyo.
Katika tathimini hiyo, Bonaventure Kagayo ambaye ni Meneja Miradi kutoka Oxfam ameshauri vikundi hivyo kuwa na malengo makubwa na endelevu kijikwamua kiuchumi kupitia kilimo “tubadilishe mitizamo yetu ya kale na tuanze kuwa wafanyabiashara , tuwe wakweli katika kutoa taarifa za mapato ya mazao yetu na kuwa na usimamizi bora wa vikundi bila kusahau kuweka kumbukumbu kwa usahihi, hii itapelekea hamasa kwa wengine ambao hawapo kwenye vikundi kuamka na kuanza biashara hii” alisema Kagayo.
Naye afisa kilimo na Usharika Katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu George Kessy amepongeza jitihada kubwa zinazofanywa na vikundi hivyo, huku akiwashauri maafisa kilimo katika kata hizo kuwafundisha njia bora za kilimo.
Aidha katika taathimini hio ya kilimo cha kitalu nyumba, Mtaalamu wa kilimo Adamu Migeto kutoka SUGECCO amewafundisha pia kilimo cha Pilipili hoho Nyekundu na Njano ambapo baadhi yao wameahidi kulima kikimo hicho kulingana na uhitaji mkubwa wa soko la zao hilo.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa