Walengwa wanaonufaika na Mpango wa kunusuru kaya maskini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu wameonesha mafanikio mbalimbali katika kujikwamu.
Mafanikio yaliyotajwa ni pamoja na kuanzisha ufugaji wa mifugo, kilimo, biashara ndogondogo, kuboresha makazi pamoja na kujiunga katika Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).
Hayo yamebainishwa na Mratibu wa TASAF Kishapu, Sospeter Nyamhanga alipozungumzia zoezi la uwezeshaji kaya maskini kwa mwezi Mei hadi Juni, 2018 huku akibainisha sh. milioni 238.45 zimenufaisha kaya 5959.
Nyamhanga alisema kuwa mpango huo ambao kwa sasa unawezesha jumla ya vijiji 78 wilayani humo unalenga kuzikwamua kaya maskini na kuweza kujitegemea.
Alisema zoezi hilo limeendelea kupata mafanikio kutokana na walengwa wengi kufanyia kazi elimu wanayopewa kuhusu matumizi sahihi ya fedha hizo wanazowezeshwa.
Mratibu huyo aliongeza kuwa kwa mujibu wa hatua za ufuatiliaji wa mara kwa mara unaofanyika katika vipindi tofauti tofauti baadhi ya kaya zimeanza kuonesha mabadiliko kimaisha.
Alifafanua kuwa kaya hizo zimetumia fedha hizo katika kuboresha maisha yao kwa kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi na hivyo kuweza kujipatia kipato.
Kwa mujibu wa Nyamhanga walengwa wameweza kununua mifugo mbalimbali ikiwemo mbuzi, kondoo na kuku huku wengine wakifanya biashara ndogondogo.
Aidha, alisema baadhi ya walengwa tayari wamebadilisha aina za makazi yao kutoka nyumba za tembe na nyasi za awali na kuanza kujenga nyumba za kisasa za bati hali inayoleta matumaini katika miradi kama hii.
“Lengo la mpango wa TASAF siku zote ni kuziwezesha kaya maskini kujikwamua kiuchumi na ndiyo maana mara kwa mara katika mazoezi haya tunatoa elimu ili kuwaelekeza namna nzuri ya kutumia fedha wanazowezeshwa,” alisisitiza.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa