Walengwa wa Mpango wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wilayani Kishapu wameishukuru Serikali kwa kuwawezesha kiasi cha sh. milioni 242.4 katika kipindi cha Septemba hadi Oktoba.
Wakizungumza wakati wa zoezi la uwezeshaji linalofanyika katika vijiji 78 wilayani humo baadhi ya walengwa hao walisema fedha wanazopokea zimewawesha kuanza kuboresha maisha yao.
Katika kijiji cha Mwasubi kata ya Bunambiyu baadhi ya walengwa walibainisha kuwa wameweza kununua mifugo ikiwemo mbuzi na kuku ambao wanawafuga na kuwaletea kipato.
Mafanikio mengine waliyobainisha walengwa hao ni pamoja na kuwanunulia sare na vifaa vya shule watoto wao katika kaya zao pamoja na kuwapeleka kliniki.
Aidha, walengwa waliongeza kuwa fedha wanazopokea kupitia TASAF zinawawezesha kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ambao unawawezesha kupata matibabu wakati wowote.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, George Kessy alisema zoezi hilo linakwenda vizuri pamoja na kuwa na changamoto za usafiri.
Aidha, Kessy alisema kuwa Ofisi yake inajitahidi kuhakikisha kuwa vijiji vyote vilivyo kwenye mpango vinafikiwa na hatimaye walengwa wote wanapata ruzuku hiyo inayotolewa na Serikali.
Mratibu wa TASAF Kishapu, Sospeter Nyamhanga alisema jumla ya walengwa 5,915 wamenufaika na fedha hizo huku zikilenga kukwamua kaya maskini na kuweza kujitegemea.
Nyamhanga aliwasisitiza walengwa hao watumie fedha wanazopata kupita mpango kwa matumizi sahihi kama ambavyo inatakiwa ili waweze kujikwamua.
Aliongeza kuwa zoezi hilo limeendelea kuwa na mafanikio kwani idadi kubwa ya walengwa wanatimiza masharti ya elimu na afya.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa