Wanavituo vya taarifa na Maarifa wa Halmashauri ya Masalala wametembelea vituo vya taarifa na Maarifa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga na kujionea namna Halmashauri hiyo ilivyofanikiwa katika uandaaji wa bajeti kwa mrengo wa kijinsia na jinsi jamii na serikali wanavyoshirikiana katika shughuli za maendeleo.
Ziara hiyo ya mafunzo ya siku tatu iliyoanza jumatatu Desemba 28, 2020 ililenga kujifunza uandaaji wa bajeti kwa mrengo wa kijinsia na umuhimu wake kupitia mradi wa usawa wa kijinsia na uwezeshwaji wanawake kiuchumi unaotekelezwa na Mtandao wa Kijinsia Tanzania (TGNP) kupitia Shirika la Watu na Makazi Duniani (UNFPA).
Ziara hiyo pia ambayo imeshirikisha Madiwani, Maafisa Maendeleo, Watendaji wa Kata na Wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu na Msalalala ilikuwa na lengo la kujenga uelewa wa pamoja kuhusu bajeti yenye mrengo wa kijinsia na umuhimu wake, kubadilishana uzoefu na mbinu mbalimbali kuwezesha ushawishi uingizwaji wa maswala ya kijinsia katika bajeti ujenzi wa vuguvugu za pamoja kupitia jamii.
Wakiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kihapu, wanaharakati hao wa haki za wanawake na watoto kupitia vituo vya taarifa na maarifa ya kata ya Shigela na Lunguya wametembelea vituo vinne vya taarifa na Maarifa wilayani Kishapu ambavyo ni vya kata ya Mwaweja, Ukenyenge, Maganzo na Songwa ambavyo ni sehemu ya vituo 9 wilayani humo ambapo vingine ni Kiloleli, Kishapu, Mondo, MwaduiLuhumbo na Bunambiyu.
Miongoni mwa mambo yaliyowafurahisha wanaharakati hao kutoka Msalala ni pamoja na ujuzi katika ujenzi wa vyoo na uanzishwaji wa vyumba vya siri kwa ajili ya wanafunzi wa kike wanapokuwa katika hedhi ambapo vyumba hivyo vina vifaa vyote vinavyohitajika ikiwemo maji na taulo za kike ‘pedi’ mafano katika shule ya msingi Bulimba iliyopo katika kata ya Ukenyenge, shule ya Sekondari Ukenyenge na shule ya Sekondari Songwa ambako kumefanyika ujenzi wa vyoo na vyumba vya siri kwa ajili ya wanafunzi wa kike wanapokuwa katika hedhi.
Hali kadhalika wemetembelea zahanati ya kijiji cha Mwaweja inayoendelea kujengwa pamoja na mradi wa maji ya Ziwa Victoria katika kata ya Ukenyengea mbao utaanza kutoa huduma hivi karibuni ili kuwapunguzia wanawake adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma ya maji.
Pia wameshuhudia ujenzi wa bweni la wanafunzi wa kike katika shule ya sekondari Ukenyenge, kuona madarasa matatu ya tokanayo na mchango wa vituo vya taarifa na Maarifa wilayani Kishapu ambavyo vimekuwa vikihamasisha jamii kushiriki katika miradi ya maendeleo badala ya kuiachia serikali ifanye kila kitu.
Mbali na kutembelea shule ya sekondari Ukenyenge pia wametembelea shule maalumu ya sekondari ya wasichana maarufu kama ‘Kishapu Wasichana Sekondari’ iliyoanzishwa mwaka 2020 ikichukua wanafunzi wa kike wilayani Kishapu wanaofanya vizuri katika mitihani yao ya darasa la saba kwa sasa ikiwa na wanafunzi 115.
Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu akiwemo Anderson Mandiya wa kata ya Ukenyenge, Abdul Ngolomole wa kata ya Songwa na Bujiku Buganga Nyanda wa tata ya Mwaweja wamesema vituo vya taarifa na Maarifa ni sehemu ya jamii kwani vinafanya kazi ya jamii kwa kuibua miradi ya maendeleo. Wamesema vituo hivyo vinatoaelimu ya umuhimu wa mwananchi kuchangia kwa hiari bila shurti katika shughuli za maendeleo kwa kushirikiana na serikali.
“Vituo vya taarifa na maarifa vimekuwa msaada mkubwa sana, vimekuwa daraja kati ya wananchi na serikali. Wanavtituo vya taarifa na Maarifa wanaturahisishia kazi sisi madiwani kutokana na ushirikiano tulionao ndio maana mnaona kila mradi tunaoanzisha unafanikiwa kwa sababu wananchi wapo tayari kushirikiana na serikali”wameongeza madiwani hao.
Nao wenyeviti wa vijiji vya Mwaweja Edward Ngoyeji na Damas Francis wa kijiji cha Songwa wamesema vituo vya taarifa na Maarifa vimechangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa mimba za utotoni na matukio ya ukatili wa kijinsia ikiwemo vipigo kwa wanawake.
Mwenyekiti wa kituo cha taarifa na Maarifa kata ya Ukenyenge, Fredina Said amesema suala la hedhi sio jambo la aibu hivyo ni vyema elimu ikatolewa kwa jamii kuanzia ngazi ya familia kuwapatia watoto wa kike mahitaji yanayotakiwa wakiwa katika hedhi na watoto wa kiume waeleweshwe kuhusu hedhi kuwa sio ugonjwa wala sio tatizo.
Mwenyekiti wa kituo cha taarifa na Maarifa kata ya Kishapu Rahel Madundo ameiomba serikali kuendelea kushirikiana na vituo vya taarifa na Maarifa kwani vimekuwa chachu ya maendeleo huku pia akiiomba TGNP kutoa mafunzo ya masuala ya jinsia kwa viongozi wa vijiji na kata ili kuongeza kasi zaidi ya maendeleo.
Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Joseph Swalala ameeleza kufurahishwa kwa jinsi madiwani pamoja na wamavituo vya taarifa na Maarifa wanavyoshirikiana na Halmashauri kutekeleza miradi ya maendeleo.
Kwa upande wake kiongozi wa msafara wa wanavituo vya taarifa na Maarifa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala, Loyce Kabanza ambaye ni mwenyekiti wa kituo cha taarifa na Maarifa kata ya Lunguya amesema ziara hiyo imekuwa na mafanikio makubwa na kwamba wataenda kuboresha zaidi kazi wanazozifanya katika Halmashauri yao.
Naye diwani wa kata ya Lunguya, Benedict Mussa na Diwani wa kata ya Shilela Philbert Elikana wamepongeza jinsi madiwani wa Kishapu wanavyoshirikiana pamoja na vituo vya taarifa na Maarifa katika Halmashauri hiyo katika kutekeleza miradi ya maemdeleo na mipango mbalimbali ikiwemo kutenga bajeti kwa ajili ya taulo za kike pamoja na ujenzi wa vyumba vya siri kwa wanafunzi wa kike.
Aidha madiwani hao wamesema mambo yanayofanywa na vituo vya taarifa na Maarifa wilayani Kishapu na serikalini ya kuigwa wakitolea mfano kuanzishwa kwa shule maalumu ya wasichana Kishapu ili kupunguza matukio ya mimba na ndoa za utotoni sambamba na kuwapunguzia umbali wa kusafiri kwenda shuleni.
Akizungumza kwa niaba ya TGNP Afisa Programu, Anna Sangai amesema vituo vya taarifa na Maarifa wilayani Kishapu pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu wamekuwa ni mfano wa kuigwa katika kutenga bajeti ya mrengo wa kijinsia wakiweka kipaumbele masuala ya kujisitiri mtoto wa kike wakati ya hedhi.
“TGNP tunao ujasiri wa kusimama kifua mbele kuizungumzia Kishapu, wamefanya kazi kubwa ya kujitolea kuleta maendeleo kwa wananchi hususani katika kutenga bajeti ya mrengo wa kijinsia ndio maana TGNP iliwapa tuzo kwa hatua hiyo. Tunaamini kabisa kuwa vituo vya taarifa na Maarifa ni daraja kubwa la wanajamii na viongozi kuelekea kwenye maendeleo. Ili kufikia malengo yaliyokusudiwa ni lazima kila mtu kwa nafasi yake atomize wajibu wake kuanzia ngazi ya familia, kijiji, kata na halmashauri kwani mabadiliko yanaanza na sisi”amesema Sengai.
“Natoa wito kwa vituo vya taarifa na Maarifa kushirikiana na wataalamu wa halmashauri kwani wana vitu vingi mnavyopaswa kujifunza kutoka kwao. Tumieni majukwaa mbalimbali kuzungumzia maendeleo na mkumbuke kuwa vituo vya taarifa na Maarifa sio upinzani bali vipo kwa ajili ya kusaidia watu katika jamii” ameongeza Sengai.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa