Wanawake wilayani Kishapu wametakiwa kusimamia malezi ya watoto wao ili kuwaepusha na vitendo vya kijinsia dhidi yao hususan vinavyochangia wapate mimba za utotoni.
Mwito huo umetolewa na Katibu Tawala Wilaya ya Kishapu, Shadrack Kengese wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kiwilaya yaliyofanyika kijiji cha Ndoleleji.
Kengese aliwataka wanawake kuwa karibu na watoto wao na kuwapatia malezi bora hususana kuwahimiza kuzingatia masomo wasijiingize katika vitendo vinavyochangia mimba.
“Akinamama mnapaswa kuwa na uchungu na watoto, tuwaonye wanapokosea tumeona wilaya yetu ina changamoto kubwa ya mimba za utotoni hasa kwa wanafunzi na watoto hao tulitegemea watimize ndoto zao lakini wanashindwa,” alisema.
Aidha, Katibu Tawala huyo alikemea tabia ya baadhi ya wazazi kuwa sehemu ya uovu kwa kutokutoa ushahidi pindi kunapotokea vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto.
Katika sehemu ya maadhimisho hayo wanafunzi wa kike wa shule ya sekondari Mangu waishio katika bweni walikabidhiwa zawadi mbalimbali zikiwemo vyakula na vifaa vya shule.
Maadhimisho hayo yalifanyika kwa ushirikiano na wadau Save the Children International, Agape, Redeso na World Vision ambapo kilele chake huwa Machi 8 ya kila mwaka.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa