Wasimamizi wakuu wa vituo pamoja na wasimamizi wasaidizi wa vituo vya kupigia kura wametakiwa kuzingatia muda wa kufungua kituo cha kupigia kura ikiwa ni pamoja na muda wa wapiga kura kuanza kupiga kura wakihakikisha orodha ya majina iliyobandikwa inafanana na majina na yaliyomo kwenye daftari la mpiga kura pamoja na kitambulisho cha mpiga kura.
Hayo yamebainishwa jana na Jackson Ruhele ambaye ni afisa uchaguzi ngazi ya kata alipokuwa anatoa semina elekezi kwa wasiamizi hao wa vituo na wasimamizi wasaidizi wa vituo vya kupigia kura katika ukumbi wa Shirecu wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga.
Ruhele alisema msimamizi wa kituo ndiye mkuu wa kituo cha kupigia kura na atakuwa na jukumu la kusimamia kura na kuhakikisha utulivu na usalama unakuwepo katika kituo cha kupigia kura.
“Wajibu wa msimamizi wa kituo ni kupokea vifaa kwa ajili ya uchaguzi katika kituo husika kuandaa na kufungua kituo cha kupigia kura vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa moja kamili asubuhi na kufungwa saa kumi jioni,”alisema Ruhele
Aidha alisema msimamizi anatakiwa kutoa ushauri na maelekezo kwa wapiga kura pale inapohitajika na kufunga zoezi mara baada ya zoezi la kupiga kura kukamilika, pia mawakala waliopo kituoni wanatakiwa kuhakikisha wanapatiwa fomu namba 14 na fomu namba 16 ambayo itawaongoza.
“Msimamizi anatakiwa kushughulikia malalamiko yanayojitokeza kituoni na Kukamilisha fomu zote za malalamiko na kukabidhi kwa msimamizi wa uchaguzi au msimamizi msaidizi”aliongeza Ruhele
Baadhi ya wasimamizi wa vituo ambao walipatiwa mafunzo Emmanuel Samweli na Juliana Maige walisema mafunzo hayo ya kuelekezwa jinsi ya kusimamia wapiga kura yatawasaidia kufanya kazi kwa weledi na ,hivyo watasimamia vizuri na watalinda amani.
Kwa upande wake msimamizi mkuu wa uchaguzi katika katika jimbo la Kishapu Emmanuel Johnson alisema wasimamizi wa vituo wapo 460, wasimamizi wasaidizi 460, na makarani waelekezi ni 460 jumla wapo 1380.
“Tumesimamia vizuri wasimamizi wa uchaguzi na wasaidizi pamoja na mawakala wa uchaguzi wamepata mafunzo vizuri kwa wakati hivyo tunaamini watasimamia vizuri na uchaguzi katika wilaya yangu utakuwa ni wa amani kabisa naendelea kusisitiza kuwa wahakikishe wanatenda haki na kulinda amani ya nchi yetu hivyo tunawaomba wananchi wenye sifa wajitokeze wote ili waweze kupiga kura”alisema Ndugu Johnson.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa