Wazazi wametakiwa kuwapatia watoto elimu bila ubaguzi na kuachana na mila potofu za kuwaozesha kabla ya wakati kuwa kwa kufanya hivyo ni kujipa laana wenyewe.
Mwito huo umetolewa na Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Kishapu, Joseph Swalala Oktoba 11, katika kijiji cha Bunambiyu wilayani Kishapu wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike.
Swalala alisema kuwa Serikali inatoa elimu bila malipo na hivyo jukumu la wazazi ni kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa kuwapatia mahitaji ya shule zikiwemo sare.
Aliwataka wanafunzi kuacha kujiingiza katika mambo yasiyofaa ambayo huchangia kupata mimba kablaya wakati huku akisisitiza jamii kuwa sehemu ya ulinzi wa mtoto wa kike.
“Tunatoa rai kwa watendaji wote wa vijiji na kata hatuna sababu ya kukaa na kesi za mimba, ni kosa mnatakiwa mripoti polisi ili hatua zaidi zichukuliwe,” alisema Swalala.
Kwa upande wake Meneja wa Shirika linalojihusiha na watoto la Save The Children Kanda ya Ziwa, Benety Malima aliwataka wazazi kuwa na ushirikiano na walimu katika kulea watoto.
Sanjari na hili meneja huyo alisisisitiza kuwa watoto wote ni sawa hivyo hakuna sababu ya kuwafanyia ubaguzi wowote hususan katika suala zima la kuwasomesha.
Alibainisha kuwa changamoto ya ukosefu wa mabweni inachangia kwa kiasi kikubwa mimba za wanafunzi katika wilaya hususan katika kata ya Bunambiyu kutokana na wanafunzi hao kuishi uraiani.
Aidha, Malima aliiomba Serikali iingilie kati na kusaidia katika kuondosha tatizo hili kwani linaathiri watoto wa kike na hivyo kukatisha ndoto zao za kusoma.
Maadhimisho hayo yamefanyika kiwilaya katika kijiji cha Bunambiyu huku kauli mbiu ikiwa ni ‘Imarisha uwezo wa mtoto wa kike; Tokomeza ukeketaji,mimba na ndoa za utotoni’.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa