Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa ametembelea na kukagua soko la pamba la chama cha ushirika cha msingi (AMCOS) kijiji cha Mwagongo alipofanya ziara wilayani Kishapu Julai 13, 2018.
Akiwa kijijini hapo Mhe. Majaliwa alizungumza na wananchi ambapo aliwataka viongozi wapya wa vyama ushirika mkoani Shinyanga kuwatumikia wananchi ili ulete tija kwa wananchi.
Aliwataka wananchi kutomvumilia kiongozi yeyote ambaye wanamuona hafai kuongoza na kuwa aachie ngazi ili nafasi hiyo ichukuliwe na mtu mwingine ambaye yuko tayari kuwatumikia.
Mhe. Waziri ambaye yuko ziarani wilayani humo alisiistiza kuwa tunataka ushirika urudishe matumaini kwa wananchi kama ilivyokuwa zamani ambapo ulimuwezesha mwananchi kuwa na maisha mazuri.
“Hapo zamani, ushirika ulimwezesha mwananchi kununua baiskeli au redio lakini kwa sasa hili haliwezekani, tunataka ushirika wa sasa ubadilike na umwezeshe mwananchi kununua gari la kutembelea ama kujenga nyumba bora,” alisema.
Awali akimkaribisha Mhe. Waziri Mkuu alikutana na wananchi, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanya, Mhe. Zainab Telack alisema kuwa zao la pamba linafanya vizuzri katika mauzo yake.
Alisema kuwa mkoa unatarajia kuvuna jumla ya tani 77,197 za pamba ambapo kuna jumla ya wakulima 44,088 wa zao hilo ikiwa ni ongezeko kutoka wakulima 28,540 ambao walikadiriwa.
Kwa mujibu wa Mhe. Telack jumla ya kilo milioni 3.3 za zao hilo kubwa katika mkoa huo hususan Wilaya ya Kishapu zimeshauzwa huku nyingine zikiwa bado shambani zikisubiri kuvunwa.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa