Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa leo Julai 13, 2018 amefanya ziara katika Wilaya ya Kishapu na kuzungumza na watumishi wa umma wilayani humo ambapo amesisitiza uwajibikaji kwa kila mmoja aendelee kutimiza wajibu wake katikia kuwahudumia wananchi.
Mhe. Majaliwa aliwapongeza watumishi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kwa kuchapa kazi pamoja na kukabiliwa na changamoto mbalimbali huku akiwatia moyo.
Aliongeza kuwa Serikali imedhamiria kupeleka huduma bora kwa wananchi na hivyo kuwataka wataalamu katika sekta mbalimbali wilayani humo kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi katika maeneo yao.
“Watumishi muwafuate wananchi kule vijijini mkasiikilize shida zao na kuizitatu, Mheshimiwa Rais amekuwa akisisitiza kuwa tuwatumikie wananchi wa kule chini na ndiyo maana ya Serikali za Mitaa na pia wakuu wa idara tuwe na mpango kazi kwa kuzingatia matakwa ya Serikali,” alisisitiza Mhe. Majaliwa.
Aidha, aliwataka kuwa na moyo wa uzalendo na kufanya kazi kwa kuwahudumia wananchi bila kujali matabaka yao huku akionya watumishi wasio kuwa waadilifu kuwa hawana nafasi katika Serikali.
Kwa upande mwingine Mhe. Waziri Mkuu aliitaka Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kushirikisha sekta binafsi katika masuala ya uwekezaji ili kuweza kuleta tija na maendeleo.
Alisema kuwa sekta hizo zina nafasi katika kuleta maendeleo kwa wananchi kwani ndizo zinajenga viwanda kama ambavyo Serikali inasisitiza na pia zinajenga miondominu ya huduma za kijamii kama vile hospitali, shule na maji.
Awali akizungumza Mbunge wa Jimbo la Kishapu, Suleiman Nchambi alimshukuru Mhe. Waziri Mkuu kwa mradi mkubwa wa maji ya Ziwa Victoria ambao kwa sasa umeweza kusaidia kupunguza changamoto ya uhaba wa wake.
Aliiomba Serikali isaidie kutoa kiasi cha sh. Milioni 250 ili ikamilishe kazi ya kusambaza maji katika maeneo ya mji mdogo wa Maganzo wilayani humo ili kuondoa kabisa kero ya maji inayowakabili wananchi.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa