Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Mhe. Josephat Limbe akizungumza kwenye Baraza la Madiwani, likilenga kujadili Taarifa za Robo ya Pili wa mwaka wa fedha 2025/2026 (Oktoba-Disemba) katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.
Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga limefanya mkutano wa kujadili taarifa za Robo ya Pili ya mwaka wa fedha 2025/2026 (Oktoba-Disemba), Januari 28, 2026 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, ambapo Waheshimiwa Madiwani wamepata nafasi ya kujadili mada mbalimbali za maendeleo sambamba na kupokea taarifa za kamati za kudumu.

Akizungumza katika Baraza la Madiwani, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Mhe. Josephat Limbe, amesema Baraza haliridhishwi na mfumo wa mnunuzi mmoja wa zao la pamba, hivyo limeazimia uwepo wa soko huria ili wakulima wanufaike zaidi na zao lao. Amebainisha kuwa mfumo wa mnunuzi mmoja umekuwa ukilalamikiwa na wakulima kutokana na changamoto za bei ndogo na kukosa ushindani, hali inayowanyima fursa ya kupata thamani halisi ya mazao yao. Kupitia soko huria, wakulimawatapata uhuru wa kuchagua wanunuzi, kuongeza ushindani na hatimaye kuinua kipato cha wananchi.

Mbunge wa Jimbo la Kishapu, Mhe. Lucy Thomas Mayenga, amewapongeza Waheshimiwa Madiwani kwa mjadala mpana na wenye tija kuhusu masuala ya maendeleo na ameahidi kufuatilia kwa karibu ili kuhakikisha suala la pamba linapatiwa ufumbuzi wa kudumu. Aidha, amesisitiza kuwa Baraza la Madiwani lina nafasi muhimu katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhakikisha changamoto zinazowakabili wananchi zinapatiwa ufumbuzi kupitia ushirikiano wa karibu kati ya madiwani, wataalamu wa Halmashauri na Serikali Kuu.

Mbunge wa Jimbo la Kishapu mkoani Shinyanga Mhe. Lucy Mayenga akizungumza kwenye Baraza la Madiwani, likilenga kujadili Taarifa za Robo ya Pili wa mwaka wa fedha 2025/2026 (Oktoba-Disemba) katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Peter Masindi, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha masuala ya lishe mashuleni akieleza kuwa lishe bora ni msingi wa maendeleo ya elimu, afya na ustawi wa watoto. Vilevile, amehimiza utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, akiwataka madiwani kuchukulia kwa uzito suala hilo na kuhamasisha wananchi kujiunga, akibainisha kuwa jukumu hilo ni la kila kiongozi na mshiriki wa mkutano huo.

Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Mhe. Peter Masindi akizungumza kwenye Baraza la Madiwani, likilenga kujadili Taarifa za Robo ya Pili wa mwaka wa fedha 2025/2026 (Oktoba-Disemba) katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Wilaya ya Kishapu, Shija Ntelezu ameweka mkazo kwenye hoja ya lishe na kuwataka madiwani kuhakikisha mpango uliowekwa unatekelezwa kwa vitendo, huku Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Wilayani humo, akilipongeza Baraza kwa jinsi lilivyoongozwa na kusisitiza kuwa kiu ya maendeleo ya Kishapu ni ya kila mtu bila kujali chama, jambo linalodhihirisha ushirikiano wa kisiasa kwa maslahi ya wananchi.


Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Wilaya ya Kishapu, Shija Ntelezu na Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Wilayani humo wakizungumza kwenye Baraza la Madiwani, likilenga kujadili Taarifa za Robo ya Pili wa mwaka wa fedha 2025/2026 (Oktoba-Disemba) katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.
Katika mkutano huo, kamati za kudumu zilizowasilisha taarifa zake ni pamoja na Kamati ya Kudhibiti UKIMWI, Kamati ya Huduma za Jamii, Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira pamoja na Kamati ya Fedha, Utawala na Mipango.




Wenyeviti na wawakilishi wa kamati za kudumu wakiwasilisha Taarifa za Robo ya Pili wa mwaka wa fedha 2025/2026 (Oktoba-Disemba) katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.
Mkutano umehitimishwa kwa wito wa madiwani na wataalamu kuibua vyanzo vipya vya mapato, kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kuendeleza ushirikiano kati ya viongozi, wataalamu na wananchi ili kupelekea kasi ya maendeleo katika Wilaya ya Kishapu.






Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu: +255282770020
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa