Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Joseph Mkude, amewataka wananchi wa Wilaya ya Kishapu na Mkoa wa Shinyanga kwa ujumla kushirikiana na vyombo vya dola katika kuripoti matukio ya ukatili wa kijinsia ili kupambana na ukatili huo na kuifanya jamii kuwa salama. Akizungumza katika maadhimisho ya Kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia, Mkude alisisitiza umuhimu wa kutoa taarifa sahihi na haraka ili kudhibiti ukatili wa kijinsia.

Afisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa wa Shinyanga, Bi. Lidya Kwesigabo, alitoa taarifa kuhusu utekelezaji wa mpango wa Mkoa wa Miaka Mitano wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto, akibainisha kwamba ofisi ya Mkuu wa Mkoa inashirikiana na mashirika ya serikali na yasiyo ya kiserikali kutoa elimu, huduma za kisheria na kuunda madawati ya ulinzi wa mtoto.

Utafiti wa Maendeleo ya Watu na Afya Tanzania (TDHS) 2022 ulionyesha kwamba matukio ya ukatili wa kijinsia mkoani Shinyanga yalipungua kutoka asilimia 34 mwaka 2010 hadi asilimia 28 mwaka 2022, ingawa juhudi za kupambana na ukatili bado zinaendelea kwa kutoa huduma za kijamii na miundombinu bora ili kuhakikisha jamii inakuwa salama.


Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu: +255282770020
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa