Mwenyekiti mpya wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu na Diwani wa Kata ya Ndoleleji Mhe. Josephat Limbe Emmanuel, akizungumza kwenye mkutano wa kwanza wa baraza la madiwani uliofanyika leo Disemba 03,2025 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.
Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kupitia baraza jipya la Madiwani limemteua Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti watakaowaongoza madiwani wateule katika kipindi kijacho. Mkutano huo umefanyika leo Disemba 03,2025 katika ukumbi wa Halmashauri hiyo, ambapo shughuli muhimu za kiutawala zimefanyika ikiwemo madiwani wateule kuapishwa, kuundwa kwa kamati za kudumu za Halmashauri na kupitisha ratiba ya vikao vya Halmashauri.
Akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi; Mwenyekiti Mteule wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu ambaye ni diwani wa kata ya Ndoleleji kupitia Chama cha Mapinduzi, Mhe.Josephat .L. Emmanuel amewashukuru madiwani wenzake kwa kumuamini kumpa nafasi hiyo na kuahidi kuongoza baraza hilo kwa uadilifu, weledi na misimamo inayojenga mustakabali wa wananchi wa Kishapu.
“Tunalo jukumu kubwa la kwenda kuwatumikia Wanamchi wetu ambao wametuamini kwa lengo kubwa la kuwapatia maendeleo, na huduma za kijamii ziwafikie popote pale walipo. Tutahakikisha tunasimamia maelekezo ya Mheshimiwa Rais na maazimio ya baraza letu” Alisema.
Aidha Mhe. Enock Reuben Bundala ambaye ni diwani wa kata ya Masanga alichaguliwa kuwa makamu Mwenyekiti wa Halmashauri.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Mhe.Peter Masindi akizungumza kwenye mkutano wa kwanza wa baraza la madiwani uliofanyika leo Disemba 03,2025 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu katika hotuba yake amewapongeza viongozi hao huku akiwakumbusha thamani ya imani waliyopewa na wananchi wa Kishapu.
“Nafasi mliyopewa ni dhamana nzito. Wajibu wenu kama madiwani ni kuhakikisha mnasikiliza na kutatua kero za wananchi. Shirikianeni na watendaji wenu, maana ninyi ndio viongozi mnaowaongoza katika maeneo mnayoyasimamia” Alisema
Mhe. Masindi amesisitiza pia viongozi hao kutojihusisha na maslahi binafsi kwenye miradi ya Serikali. “Vunjeni makundi ya kisiasa yaliyokuepo kabla ya uchaguzi ili mkumbatie wawekezaji. Zingatieni mipaka ya utendaji. Tunataka Kishapu iwe mfano wa utawala bora.” Ameongeza Mhe. Masindi.
Makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu na diwani wa kata ya Masanga Mhe. Enock .R. Bundala akizungumza kwenye mkutano wa kwanza wa baraza la madiwani uliofanyika leo Disemba 03, 2025 katika ukumbi wa Halmashauri hiyo.
Naye, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kishapu Bi. Fatma Mohamed, aliyekuwa mwenyekiti wa muda wa kikao kabla ya kuapishwa na kuchaguliwa kwa Mwenyekiti mpya, amewapongeza madiwani hao kwa kukamilisha uchaguzi na kuwataka waende kwenye hatua ya utekelezaji.
“Wananchi wamewachagua kwa imani kubwa. Huu sio wakati wa maneno tena ni wakati wa kazi. Tekelezeni yale mliyoyaahidi wakati wa kampeni.” Amesema.

Katibu Tawala Wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, Bi. Fatma Mohammed akizungumza kwenye mkutano wa kwanza wa baraza la Madiwani uliofanyika Disema 03,2025 katika ukumbi wa Halmashauri hiyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Ndg. Emmanuel Johnson amewataka madiwani kuimarisha ushirikiano katika ngazi zote za utendaji ili kujenga mazingira mazuri ya kazi.
“Ili tujenge Kishapu tunayoiota ni lazima tushirikiane. Fanyeni maamuzi kwa kuzingatia mapato halisi ya Halmashauri, na tumieni busara katika kushughulikia makosa ya Watumishi. Mko hapa kuwaongoza, kuwashauri na kuwaweka kwenye mstari”. Amesema Mkurugenzi
Pia amewakumbusha umuhimu wa kuzifahamu kwa kina kanuni, taratibu na sheria za Halmashauri pamoja na kanuni za Utumishi wa Umma ili kuhakikisha utendaji wenye uwazi na uadilifu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Ndg. Emmanuel Johnson akizungumza kwenye mkutano wa kwanza wa baraza la madiwani uliofanyika Disemba 03,2025 katika ukumbi wa Halmashauri hiyo.
Katika hatua nyingine, madiwani wapya 40 waliapishwa,ambapo madiwani 8 kati ya hao ni wa viti maalumu,huku Hakimu Mkazi Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Bi. Johanitha Projest akiratibu zoezi hilo na kisha kuunda kamati za kudumu za Halmashauri ambazo ndizo muhimili wa utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo.
Hakimu mkazi Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Bi. Joanitha Projest akiongoza zoezi la kutoa viapo kwa madiwani wateule,Disemba 03,2025 katika ukumbi wa Halmashauri hiyo.


Baadhi ya Madiwani wateule kutoka katika kata mbalimbali za Wilaya ya Kishapu wakila kiapo mara baada ya kuapishwa na Hakimu Mkazi Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, leo Disemba 03,2025 katika ukumbi wa Halmashauri hiyo.
Aidha Mkutano huu wa baraza la kwanza la madiwani umeudhuriwa na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kishapu, mwakilishi wa Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga, wajumbe wa Tume ya Uchaguzi, Taasisi za kifedha za benki ya NMB na CRDB pamoja na watumishi Wakuu wa idara na vitengo wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu: +255282770020
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa