
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Mhe. Peter Masindi akizungumza na wananchi wa Ngofila wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa ununuzi wa pamba katika vyama vya msingi na kufanya mkutano wa hadhara Ngofila lengo ikiwa ni kufuatilia mafanikio na changamoto za msimu wa ununuzi wa pamba ili kuhakikisha mnyororo wa masoko unakwenda vizuri bila kukwamishwa na ukiukwaji wa taratibu wa ununuzi.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Mhe. Peter Masindi ameagiza kampuni ya Aham Limited kushusha tani 30 za pamba zilizonunuliwa kinyume na taratibu kutoka Chama cha Msingi cha Kiloleli (Amcos), akisisitiza kuwa ununuzi huo ulifanyika kwa kutumia mizani isiyo rasmi na hivyo kukiuka kanuni za ununuzi wa zao hilo.
Akizungumza Juni 3,2025, wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa ununuzi wa pamba katika vyama vya msingi vya Mwamashele, Mwamanota, Inolelo (Amcos ya Raha ya Balimi), Ngofila, Kalitu na Kiloleli na kufanya mkutano wa hadhara Ngofila, Mhe. Masindi amesema lengo ni kufuatilia mafanikio na changamoto za msimu wa ununuzi wa pamba ili kuhakikisha mnyororo wa masoko unakwenda vizuri bila kukwamishwa na ukiukwaji wa taratibu.
"Aham amenunua pamba kupitia mzani ya kawaida badala ya mzani wa kidijitali kama inavyotakiwa, kuanzia sasa naagiza pamba yote ishushwe na ipimwe upya kwa kutumia mzani wa kidijitali ili kuwezesha serikali kupata mapato stahiki na taarifa sahihi kwa Bodi ya Pamba," amesema Masindi.
Ameeleza kuwa matumizi ya mizani isiyo rasmi yanapotosha takwimu muhimu kwa Halmashauri, husababisha kukosekana kwa makadirio sahihi ya ushuru wa 3% kwa kilo moja, na hata kuathiri taarifa za idadi ya wakulima husika jambo ambalo ni muhimu kwa maandalizi ya msimu ujao kwa bodi ya pamba vilevile, ameonya kuwa mkulima huenda akapunjwa, huku mnunuzi akijikuta akikumbwa na adhabu za kusafirisha mazao bila vibali halali.

Katika hatua nyingine, kufuatia malalamiko kutoka kwa wakulima wa Kata ya Ngofila kuhusu kucheleweshwa kwa malipo Masindi amemuelekeza mnunuzi kutoka Lugeye Company Limited anayenunua pamba katika vyama vya msingi vya Mwamanota, Ngofila na Kalitu kuhakikisha anawalipa wakulima wote kwa wakati.
"Mpango wa serikali ya awamu ya sita ni kuhakikisha mkulima ananufaika hivyo kama mnunuzi hana fedha za kulipa, apishe mnunuzi mwingine hatutaki ucheleweshaji wa malipo wala ubadhirifu wowote kwenye mizani na wote wanaonunua pamba kwenye maeneo husika waende kwa wakati kama kuna sababu nyingine watueleze mapema ili turuhusu wanunuzi wengine kuendelea na ununuzi pamba" amepngeza kwa msisitizo.

Mkuu huyo wa Wilaya pia amewasihi wakulima kuuza pamba kwenye vyama vya msingi pekee huku wakijiwekea mipango ya muda mfupi, kati na mrefu kwa ajili ya kuboresha maisha yao kupitia zao la pamba akiwakumbusha umuhimu wa kuwekeza katika elimu ya watoto wao,kuweka akiba ya fedha na vyakula, ujenzi wa nyumba bora na uzingatiaji wa lishe bora kutokana na fedha watakazozipata.
"Mwanaume aliyefanikiwa huwa na mwanamke nyuma yake hivyo msitumie fedha za pamba kwa 'nzige' (wanawake wauzao miili yao) watamaliza fedha zenu na kuwaachia magonjwa, mwisho wake mtawatesa wake na watoto wenu",ameongeza.
Masindi ameeleza kuridhishwa na mwenendo wa ukusanyaji wa pamba huku akihimiza wakulima kuuza pamba safi ili wapate bei nzuri na kuhakikisha vyama vya msingi vinafuata maelekezo ya serikali na Bodi ya Pamba katika ununuzi na uuzaji.
Mwakilishi wa Kampuni ya ununzi wa pamba ya Lugeye, Juni Butina akizungumza kuhusiana na ucheleweshwaji malipo kwa wakulima amesema changamoto iliyotokea ni ucheleweshwaji wa taarifa ya kuomba fedha kutoka kwa viongozi wa Amcos ili waletewe kwa wakati lakini kampuni hiyo itahakikisha inafuata taratibu zote za ununuzi walizoelekezwa na serikali ya Wilaya na bodi ya pamba.
Takwimu za Ukusanyaji Pamba (Hadi Juni 3, 2025)
Mwamashele Amcos Tani 7 Mnunuzi ni Bioustain Tanzania Ltd,Mwamanota Amcos Tani 12,Inolelo (Raha ya Balimi) Tani 14,Ngofila & Kalitu Amcos zaidi ya Tani 10Mnunuzi ni Lugeye Company Ltd pamoja Kiloleli Amcos zaidi ya Tani 50 na Mnunuzi ni Aham Company Limited.
Mnamo mwezi Mei,15,2025 Mkuu wa Wilaya ya Kishapu alizindua msimu mpya wa pamba 2025/2026 kwa ngazi ya Wilaya akikutana na wadau mbalimbali wa zao hilo ambapo masuala muhimu yalizungumziwa kuhusu bei,mizani,ubora wa pamba,uuzaji na ununuzi ambapo pamba safi itauzwa kwa bei elekezi ya Tsh. 1,150 kwa kilo, huku pamba fifi ikiuzwa kwa Tsh. 575 kwa kilo.

Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu: +255282770020
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa