Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepanga kutumia Dola za Marekani milioni 77.4, sawa na Shilingi Bilioni 208.9, kuziwezesha kaya duni 260,000 zinazojishughulisha na kilimo na uvuvi. Mpango huu unalenga kuwajengea uwezo kitaalamu wananchi hao na kuwaunganisha na taasisi za kifedha, hususan Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), kwa kipindi cha miaka sita mfululizo ili kuwaimarisha kiuchumi kupitia uzalishaji wa mazao ya kilimo na uvuvi.

Kaya hizo, ambazo zinakadiriwa kuwa na takriban Watanzania milioni 1.3, zipo katika mikoa 11 ya Tanzania Bara, na zitafaidika kupitia Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (Agriculture and Fisheries Development Programme - AFDP). Mradi huu unalenga kuimarisha mifumo jumuishi ya usalama wa chakula na lishe katika halmashauri 41 ndani ya mikoa hiyo.

Ili kuhakikisha utekelezaji thabiti wa programu ya AFDP, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu inayoratibu utekelezaji kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI, imewakutanisha Makatibu Tawala wa mikoa yote 11 pamoja na maafisa ugani kutoka halmashauri husika katika kikao kazi maalum kinachoendelea mkoani Morogoro. Lengo ni kujenga uelewa wa pamoja kuhusu utekelezaji wa programu hiyo.

Akifungua kikao hicho, Mkurugenzi wa Tawala za Mikoa kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Bi. Beatrice Kimoleta, aliwataka watendaji hao kusimamia kwa umakini matumizi ya fedha za mradi, akisisitiza kuwa hazipaswi kutumika kinyume na taratibu.
“Nasisitiza kuwa fedha hizi zisitumike kinyume na taratibu zilizowekwa katika utekelezaji wa programu hii. Serikali inatarajia kuona matokeo chanya. Isitokee hata senti moja ikatumika nje ya matumizi yaliyokusudiwa. Kufanya hivyo ni sawa na kuwadhulumu walengwa, jambo ambalo halitavumiliwa,” alionya Bi. Kimoleta.
Awali, Mratibu wa Programu ya AFDP, Bw. Salimu Mwinjaka, alitaja mikoa itakayofaidika na mradi huo kuwa ni Morogoro, Manyara, Singida, Dodoma, Tabora, Mwanza, Lindi, Pwani, Shinyanga, Geita na Tanga.
Akiainisha matarajio ya programu hiyo ifikapo mwisho wa utekelezaji wake, Bw. Mwinjaka alisema Serikali inalenga kuwa na meli zake za uvuvi katika Bahari ya Hindi, kuendeleza zao la mwani kwa wananchi wa visiwani Zanzibar, kupunguza upotevu wa mazao ya samaki, kuongeza upatikanaji wa mbegu bora za mazao kama mahindi, alizeti na jamii ya kunde, pamoja na kuanzisha viwanda vya uzalishaji wa chakula cha samaki, hatua itakayochochea uzalishaji wa vifaranga bora vya samaki.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu: +255282770020
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa