Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya Kishapu Bw.Joseph Swalala, akizungumza katika hafla ya utoaji wa mikopo kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Wenye Ulemavu iliyofanyika leo Januari 29, 2026 katika ukumbi wa Halmashauri hiyo.
Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu imefanya hafla maalum ya utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu vilivyopo katika Halmashauri hiyo, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Serikali la kuwawezesha kiuchumi makundi maalum katika jamii.
Hafla hiyo imefanyika leo Januari 29, 2026 katika ukumbi wa Halmashauri hiyo na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa wakiwemo maafisa maendeleo wa Kata, Wataalamu wa Idara ya Mendeleo ya Jamii ngazi ya Halmashauri, Mwenyekiti wa Kamati ya Uhakiki wa Mikopo ngazi ya wilaya, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Kishapu, Taasisi za kifedha za CRDB na NMB pamoja na wanufaika wa mikopo hiyo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Peter Masindi ambae ndio alikuwa mgeni rasmi alisema kuwa mikopo hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya sita ya Rais. Dkt. Samia Suluhu Hasaan katika kuimarisha uchumi wa wananchi na kupunguza umasikini.
Aliongeza kuwa vikundi vinavyopokea mikopo hiyo vinapaswa kutumia fedha hizo kwa umaminifu na kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuleta matokeo chanya katika kaya zao.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Peter Masindi akizungumza katika hafla ya utoaji wa mikopo kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Wenye Ulemavu iliyofanyika leo Januari 29, 2026 katika ukumbi wa Halmashauri hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii Halmashauri Kishapu Bw.Joseph Swalala ambaye alimuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, alieleza kuwa jumla ya Sh.milioni 304,843,277 kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri zilitengwa kwa ajili ya mikopo ya vikundi kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ikiwa ni awamu ya kwanza. Amesema jumla sh. Milioni 186,500,000 zimetolewa, ambapo sh. Mil. 75,000,000 ni kwa vikundi 10 vya wanawake na sh. Mil. 111,500,000 ni kwa vikundi 11 vya vijana.
Aidha amebainisha kuwa kwa Kundi la watu wenye ulemavu hawakuweza kunufaika na mikopo hiyo kwa sababu ya kutokukidhi kwa baadhi ya vigezo na vielelezo vinavyohitajika.
Ameongeza akisema kuwa mikopo hiyo haina riba ana inalenga kukuza kipato cha mnufaika, hivyo inatakiwa kurejeshwa kwa wakati ulioainishwa.Amesisitiza mikopo hiyo ikatekeleza miradi ya vikundi husika waliyoianzishwa na sio vinginevyo ili kufuikia lengo walilokusudia.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu akizungumza katika hafla ya utoaji wa mikopo kwa Wanawake, Vijana na Wenye Ulemavu iliyofanyika leo Januari 29, 2026 katika ukumbi wa Halmashauri hiyo.
Naye,Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mhe. Josephat Limbe ametoa wito kwa wanawake na vijana wa vikundi hivyo kujiwekea mikakati endelevu, thabiti na kuwa waadilifu katika kukamilisha malengo na ndoto zao walizojiwekea kupitia fedha za mikopo hiyo.

Baadhi ya wanufaika wa mikopo wakiwemo Wanawake na Vijana wakisikiliza hotuba za viongozi mbalimbali katika hafla ya utoaji mikopo iliyofanyika leo Januari 29, 2026 katika Ukumbi wa Halmashauri hiyo.


Kwa upande wao, wanufaika wa mikopo hiyo wameishukuru Serikali chini ya Rais Samia kwa kuwapatia fursa ya kujiinua kiuchumi kupitia fedha hizo, huku wakiahidi kuboresha miradi ya biashara waliyoianzisha.
Hafla hiyo ilihitimishwa kwa zoezi la kusaini mikataba na kukabidhiwa nyaraka muhimu za mikopo baina ya vikundi hivyo.


Mkuu wa Wilaya ya Kishapu akiwa ameshika hundi ya mfano katika hafla ya utoaji mikopo kwa Wanawake, Vijana na Wenye Ulemavu iliyofanyika Januari 29,2026 katika Ukimbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.


Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu: +255282770020
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa