Watabibu wa vituo 15 vya kutolea huduma za afya katika Wilaya ya Kishapu wamepatiwa mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo kuhusu matumizi sahihi ya mfumo wa umeme jua uliofungwa katika vituo hivyo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa msaada wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na watoto (UNICEF).
Mafunzo hayo yamefanyika leo tarehe 14 Mei 2025, katika ukumbi wa Hospitali ya Wilaya ya Kishapu Dkt. Jakaya Kikwete, yakihusisha wataalamu wa afya kutoka vituo mbalimbali vya huduma ya afya. Mafunzo yamelenga kuwawezesha wahudumu wa afya kutumia kwa ufanisi mifumo ya nishati ya jua kwa ajili ya kuendesha vifaa vya kitabibu, kuhifadhi dawa zinazohitaji ubaridi, pamoja na kuwezesha huduma za usiku na dharura.

Mkufunzi mkuu wa mafunzo hayo, Bw. George Michael, kutoka kampuni ya Solar AG Energies, alieleza kuwa elimu waliyoitoa inalenga kuleta mabadiliko ya kweli katika utoaji wa huduma. “Mfumo wa umeme jua una faida nyingi hasa katika maeneo ya vijijini. Tunataka kuhakikisha kwamba kila mhudumu wa afya anaujua vyema mfumo huu, na anaweza kuutumia na kuufanyia matengenezo madogo pasipo usumbufu,” alisema Bw. Michael.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Dkt. Joseph Stephano Bahati, ambaye pia alikuwa mratibu wa mafunzo hayo, alieleza kuwa mradi huo ni hatua kubwa katika kuimarisha huduma bora za afya vijijini. “Tunashukuru sana kwa msaada huu wa UNICEF. Kupitia mafunzo haya, tunategemea maboresho makubwa katika huduma za afya hususan katika usimamizi wa vifaa vya kitabibu vinavyotegemea nishati ya umeme,” alisema Dkt. Bahati.

Msimamizi wa mafunzo hayo, Mhandisi Fredy Peter, ambaye ni mhandisi wa wilaya ya Kishapu, alieleza kuwa usimikaji wa mifumo ya umeme jua katika vituo 15 vya afya ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa serikali wa kutumia nishati jadidifu katika huduma za jamii. “Tulihakikisha kwamba mifumo iliyofungwa ni ya kisasa na yenye uwezo mkubwa wa kuhifadhi umeme kwa muda mrefu. Sasa tunawapa watumiaji uwezo wa kuisimamia vyema,” alieleza Mhandisi Fredy.

Mafunzo haya yanaakisi dhamira ya serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata huduma bora za afya, bila kujali eneo analoishi. Kupitia ushirikiano huu na UNICEF, Wilaya ya Kishapu imepiga hatua muhimu katika kuhakikisha vituo vyote vya afya vinapata nishati ya uhakika, jambo ambalo litaongeza ufanisi na kuokoa maisha ya wananchi wengi
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu: +255282770020
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa