Shirika lisilokuwa la kiserikali WAYDS, kwa kushirikiana na GAET na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Imeipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kwa hatua iliyopiga katika kutekeleza mapendekezo ya changamoto zilizoibuliwa Mwaka 2023 kwenye zahanati ya Kijiji cha Ngunga - Talaga 

Katika kikao kilichofanyika Oktoba 31, 2024, Mkurugenzi wa WAYDS, Charles Deogratius, alieleza kuwa serikali imesaidia kwa asilimia 80 katika kutekeleza mapendekezo hayo. Alibainisha kuwa wamefanya uchambuzi wa nyaraka za halmashauri na kutembelea zahanati hiyo ili kuhakikisha wananchi wanashirikishwa.

Deogratius alisisitiza kuwa walitunga kamati ya wajumbe sita kutoka sekta mbalimbali na walizingatia mambo muhimu kama mipango, usimamizi wa matumizi, na uwajibikaji. Aliongeza kuwa, kwa sasa, zahanati inatoa huduma za uzazi na inafanya vizuri katika uagizaji wa dawa, ingawa bado kuna changamoto kama ukosefu wa samani na watoa huduma wa afya.

Bi. Catherine Kalinga wa GAET alishauri halmashauri kutangaza nafasi za kujitolea kwa wahitimu wa sekta ya afya, huku akihimiza ushirikiano na wadau mbalimbali. Fredina Said, mratibu wa vituo vya taarifa, alisisitiza umuhimu wa kusogeza huduma za mafuta kwa watu wenye ulemavu wa ngozi ili kuwasaidia kwa urahisi.

Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri, Joseph Swalala, alikiri changamoto zilizopo na kuahidi kuzitatua, huku akitoa wito kwa wadau kusaidia. Dkt. Joseph Bahati, mganga mkuu wa Wilaya, aliahidi kushughulikia masuala ya samani na kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya.

Mwenyekiti wa kamati ya huduma za jamii, Mhe. Richard Dominico, aliwashukuru wadau wote kwa ushirikiano wao katika kuboresha huduma za afya katika Kijiji cha Ngunga, akisisitiza kuwa elimu zaidi inahitajika ili wananchi waweze kushiriki kikamilifu.


Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu: +255282770020
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa