Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga imeanza rasmi maandalizi ya mapokezi ya Mbio za Mwenge wa Uhuru, unaotarajiwa kupokelewa kwa shangwe na nderemo mnamo tarehe 8 Agosti 2025 katika eneo la Maganzo.

Akizungumza kuhusu maandalizi hayo, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mheshimiwa Peter Masindi, amewakaribisha wananchi wote kushiriki kikamilifu katika tukio hilo la kitaifa lenye lengo la kuhamasisha maendeleo, mshikamano na uzalendo miongoni mwa Watanzania.

Baada ya mapokezi rasmi, kutakuwa na mkesha maalum katika Viwanja vya Shirecu vilivyopo Mhunze, ambapo wananchi watajumuika pamoja kwa burudani mbalimbali ikiwa ni pamoja na ngoma za asili, vikundi vya muziki na sanaa, michezo ya kuigiza, pamoja na ujumbe maalum wa Mwenge wa Uhuru.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Bw. Emmanuel Johnson, amesema maandalizi yanaendelea kwa kasi ili kuhakikisha ushiriki mpana wa wananchi na taasisi mbalimbali katika tukio hilo. Amesisitiza kuwa Mwenge wa Uhuru sio tu ishara ya historia, bali ni chombo muhimu cha kuhamasisha ushiriki wa jamii katika shughuli za maendeleo.
Kauli mbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2025 ni:
“Jitokeze Kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa Amani na Utulivu.”

Kauli mbiu hii inalenga kuhamasisha Watanzania wote kushiriki kwa wingi katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu, kwa njia ya amani, ustaarabu na uzalendo.
Wananchi wote wa Kishapu na maeneo ya jirani wametakiwa kujitokeza kwa wingi ili kuupokea Mwenge wa Uhuru, kushiriki katika mkesha wa kitaifa, na kuonesha mshikamano wa pamoja katika kuijenga Tanzania yenye amani na maendeleo.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu: +255282770020
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa