Imebainika kuwa wanawake wengi hawatoi taarifa kwa sababu ya kuogopa kuachwa na mume wake na kuwaacha watoto wake wakiteseka. Mwanajamii mmoja alisema “ukienda kutoa taarifa ukirudi tu nyumbani unakutana na vitu vyako nje na ameshaleta na mwanamke mwingine”, hii pia inachangiwa na utaratibu na tamaduni za wasukuma hawapendi kutoa taarifa au kumshitaki mume kwa watoa huduma kama Maafisa Ustawi, polisi na mahakama badala yake wanataka kesi iishie ngazi ya familia tu.
“Ukatili dhidi ya watoto hususani mimba na ndoa za utotoni kushamiri imeelezwa kuwa ni kutokana wanajamii hawatoi taarifa kwa watoa huduma ndani ya masaa 72 hivyo kupelekea ushahidi kupotea na iwapo matukio hayo yameripotiwa basi kesi zinazofika mahakamani ni chache na zile zinazopata ufumbuzi ni chache zaidi, pia kuahirishwa kwa kesi mara kwa mara mahakamani hupelekea wahanga wa ukatili kuamua kuyamaliza kifamilia.”Haya yamesemwa na Afisa Tathimini na Ufuatiliaji kutoka Shirika la KIVULINI Godfrey Paschal wakati akiwasilisha taarifa ya upatikanaji wa haki kwa wahanga wa ukatili dhidi ya wanawake na watoto leo Desemba 04, 2019.
Afisa huyo amewataka wadau mbalimbali kutoka mashirika binafsi na serikali kushirikiana kwa pamoja kuendelea na juhudi za kutokomeza ukatili huu kwa kutoa elimu stahiki kwa jamii. Pia polisi na mahakama kushirikiana bega kwa bega na wahanga kwa kufanya upelelezi kwa muda unaotakiwa na kutoa hukumu kulingana na sheria.
Naye mkuu wa kituo cha polisi SP. Ildefonce Bernard Kagaruki amewapongeza shirika la KIVULINI kwa kazi waliyoifanya ya utafiti juu ya ukatili wa kijinsia na kuwataka wazidi kushirikiana na kamati za kiusalama wilayani Kishapu ili kutokomeza kabisa ukatili dhidi ya wanawake na watoto. “kutokana na takwimu za kiusalama, ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto kwa matukio yaliyoripotiwa kwa mwaka 2019, jumla matukio ya ukatili katika wilaya ya Kishapu yalikuwa ni 85 ambapo matukio 56 yalikuwa ni kuwapa mimba wanafunzi na ubakaji ni matukio 29. Hivyo kila mtu kwa nafasi yake asimame kupinga hii hali ya ukatili kuanzia majumbani, mashuleni mahakamani, maofisini, mahospitalini, ofisi za vijiji na kata, na mashirika yote”.
Wanajamii tusimamie na kuzingatia madili yetu yaliyokuwepo kwa watoto wetu kwa kuwapa malezi bora kutoka ngazi ya familia hadi mashuleni kwa kuanziasha klabu mbalimbali juu ya kupinga masuala ya ukatili. Hayo yamesemwa na Afisa Maendeleo ya Jamii wilaya ya Kishapu Rehema Edson.
Nao wadau mbalimbali walioshiriki katika kikao hicho wametumia fursa hio kujadili njia mbalimbali za kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto kuwa, malezi ya watoto yarudi kwenye jamii ili kushirikiana kwa pamoja na wazazi kutekeleza jukumu la malezi kwa watoto wetu, kutunga sheria ndogo ndogo kuhusu masuala ya ukatili na hatua za kisheria kufuatwa kwa watakaotoa na kupokea rushwa ili kufanikisha juhudi za kutotokomeza ukatili wa kijinsia, pia elimu izidi kutolewa kwa wanajamii juu ya ukatili wa kijinsia.
Na Catherine J. Ngowi
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa