Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Subira Mgalu amesema Serikali itaendelea na usambazaji wa nishati ya umeme katika vijiji vyote 50 katika Wilaya ya Kishapu kama ambavyo iliahidi.
Amesema hayo leo wilayani humo wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ilipofanya ziara wilaya Kishapu kukagua miradi ya umeme inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Kamati hiyo ikiwa kwenye vijiji vya Negezi na Bulimba ikiambatana pia na uongozi wa Mkoa na Wilaya, Mhe. Mgalu alisema kuwa mpango wa usambazaji umeme ni wa awamu na kuwa wananchi wasiwe na hofu kila kijiji kitafikiwa na mradi.
Aliongeza kuwa vijiji 33 kati ya 50 vitapata umeme wa REA awamu hii ya tatu wakati 17 vitapata nishati hiyo kupitia njia kuu inayounganisha mikoa ya Iringa, Dodoma, Singida na Tabora.
Kwa upande wake, Kamati hiyo ya Bunge ilisema wataendelea kuikumbusha Serikali iendelee kutimiza ahadi zake kwa wananchi za kukamilisha miradi ya umeme.
Iliwataka wananchi ambao wamepitiwa na miradi hii katika vijiji vyao kuichangamkia fursa na kuomba kuunganishiwa ili kupata huduma hiyo na kujiletea maendeleo.
Aidha iliwataka wananchi kuboresha aina za makazi yao kadiri ya uwezo wao na kuezeka nyumba zao kwa bati na kuachana na matembe na hatimaye kuwa na nyumba zilizo bora.
Katika ziara hiyo kijiji cha Bulimba kilichopo kwenye kata ya Ukenyenge kumezinduliwa rasmi huduma ya umeme mradi uliokamilshwa kupitia REA na hivyo kutarajiwa kuwanufaisha wananchi.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa