Wana vituo vya Taarifa na Maarifa kutoka katika Halmashauri ya Wilaya ya Masalala kata zaShilela na Lunguya wametembelea Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kwa ajili ya kujifunza kuhusu uandaaji wa bajeti ya mrengo wa Kijinsia na umuhimu wake kupitia maradi wa Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi unaotekelezwa na Mtandao wa Kijinsia Tanzania (TGNP)kwa kupitia Shirika la Watu na Makazi Duniani (UNFPA).
Ziara hiyo ya siku yatu itakayo husisha kutembelea vituo vya taarifa na maarifa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu imeanza leo jumatatu Desemba 28, 2020 kwa wanavituo vya taarifa na maarifa kutoka wilaya za Msalala na Kishapu kukutana katika kikao kilichofunguliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Emmanuel Johnson.
Afisa Programu kutoka TGNP, Anna Sangai amesema lengo la ziara hiyo ni kujenga uelewa wa pamoja kuhusu bajeti yenye mrengo wa Kijinsia na umuhimu wake pamoja na kubadilishana uzoefu na mbinu wezeshi ili kushawishi uingizwaji wa maswala ya jinsia katika bajeti na ujenzi wa vuguvugu la pamoja kupitia jamii.
“Kupitia Mradi wa Usawa wa Kijinsia na uwezeshaji wanawake kiuchumi pia katika ziara hii tutapitia maeneo ambayo viongozi na jamii wamefanikiwa kushawishi uingizwaji wa bajeti ya kijinsia” alisema Sangai.
Alisema bajeti yenye mrengo wakijinsia ni bajeti itakayoweza kutatua changamoto za makundi yote katika jamiii na kotoa haki kwa wote na kwamba ni lazima makundi yote katika jamii yafaidi keki ya Taifa.
Akifungua kikao hicho Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Emmanuel Johnson aliishukuru TGNP kwa kazi inayoendelea kuifanya katika jamii kwa kuhamasisha masuala ya usawa huku akibainisha kuwa Halmashauri yake inatenga bajeti kwa mrengo wa kijinsia.
Alisema matunda ya TGNP na vituo vya taarifa na maarifa yanaonekana ambapo maswala ya usawa wa kijinsia yanapewa kipaumbele katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu ili kufikia usawa wa kijinsia kwa asilimia 50 kwa 50.
“Lakini wanaume wasibaki nyuma katika kufikia usawawa 50 kwa 50. Tunapozingumzia jinsia tunazungumzia jinsi zote yaani mwanamke na mwanaume. Kama tukimsemea sana mama na kumwacha baba huenda jitihada zisifanikiwe. Jamii pia inatakiwa kuzingatia masuala ya usawa wa kijinsia na kwamba sasa hakuna jambo la mwanamke tu au mwanaumetu” alisema Johnson.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Joseph Swalala alisema licha ya Halmashauri hiyo kuzingatia maswala ya Usawa wa Kijinsia pia alibainisha kuwa wana endelea kupigana na changamoto ya mimba za utotoni kwani wameanzisha shule maalumu kwa ajili ya wasichana iitwayo ‘Kishapu Wasichana’.
Naye Diwani wa Kata ya Songwa, Abdul Ngolomole alisema mfumo wa Vituo vya Taarifa na Maarifa vinachangia kuleta maendeleo kwa kasi kubwa katika jamii.
“Vituo vya Taarifa na Maarifa vinamsaada mkubwa kwani wananchi wanakuwa sehemu ya kuibua vipaumbele na mahitaji yaliyopo katika jamii. Ushirikishwaji wawananchi umekuwa mkubwa katika maswala ya maendeleo” Alieleza Ngolomole.
Hata hivyo Mwenyekiti wa Vituo vya Taarifa na Maarifa Wilayani Kishapu, Rachel Madundo aliwashauri wanavituo vya taarifa na maarifa na maarifa kufanya kazi kwa kujituma huku wakihakikisha wanashirikiana na kutunza siri hali itakayo wafanya kuaminika katika jamii na kufanikiwa katika harakati zao.
Madundo alitumia fursa hiyo kuiomba TGNP kuongeza vituo vya taarifa na maarifa wilayani Kishapu kutokana na wilaya hiyo kuwa kubwa kigeografia na kuwa na mahitaji mengi pia.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Lunguya, Benedicto Mussa na Mwenyekiti wa kituo cha taarifa na maarifa kata ya Lunguya na Joyce Kabanza kwa niaba ya wanavikundi vya taarifa na maarifa wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala waliishukuru TGNP kwa kuandaa ziara hiyo wakielezea kuwa itawasaidia kuwajengea ujasiri zaidi utakaowasaidia kufanya kazi zao vizuri.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa