Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameziagiza halmashauri za wilaya nchini kuhakikisha zinasimamia kikamilifu kilimo cha zao la pamba ili kiwe na tija.
Ametoa agizo hilo katika kikao na wadau wa pamba kilichofanyika mjini Shinyanga ambapo alizitaka halmashauri hizo kuratibu shughuli za kilimo hicho kwa kuwapangia ratiba maafisa ugani kuwatembelea wakulima kuwapa elimu.
Akizungumza katika kikao hicho kilichoikutanisha mikoa zaidi ya 10 inayolima pamba aliwataka watendaji wakuu wa halmashauri hizo kuhakikisha kila kata na kijiji kunawepo na maafisa ugani ili wasimamie kikamilifu kilimo.
Majaliwa aliwataka maafisa ugani waliopo katika halmashauri hizo kuwafikia wakulima mashambani ili kuwapa elimu na kutatua changamoto zinazowakabili kuhusu kilimo hususan cha pamba.
“Tunataka kuhahakikisha pamba inaleta heshima na inaongeza mapato ya mkulima mmoja mmoja na hata taasisi zetu yaani halmashauri na mikoa zinaingiza mapato kupitia zao la pamba hivyo kila mmoja awajibike,” alisisitiza.
Pia, aliagiza pia ziweke mpango kazi wa namna ya kukiletea mafanikio kilimo hicho huku akisisi kuwa na kwamba atafanya ziara kukagua akisema atataka apewe taarifa ya maendeleo ya kilimo hicho.
Aidha alizitaka halmashauri kuwa na takwimu za misimu ya pamba na ziwe zimehifadhiwa vizuri kwenye kompyuta ili popote zikihitajika zipatikane kwa urahisi.
“Tumejipanga kusimamia zao la pamba kwani awali uzalishaji haukuwa mzuri mkulima anatumia nguvu nyingi sasa tutasimamia kikamilifu kuanzia maandalizi hadi masoko,” alisema Majaliwa.
Katika hatua nyingine aliwataka wadau wa kilimo cha pamba maarufu kama dhahabu nyeupe watimize wajibu ili kukifanya kiwe na tija hivyo kuinua uchumi.
Majaliwa pia aliagiza wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) kujipanga na kuelekeza kuhusu dawa zilizo bora kwa ajili ya zao hilo na Bodi ya Pamba iwajibike kufuatilia maendeleo yake.
Mkutano huo umewakutanisha pia mawaziri wenye dhamana ya Kilimo, Dk. Charles Tizeba, Viwanda na Uwekezaji, Charles Mwijage, wakuu wa mikoa, wilaya, makatibu tawala, wabunge, wakurugenzi wa halmashauri, taasisi za kilimo, wakulima na wanunuzi wapamba.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa