Shirika la OPE (Organization of People Empowement) wamefanya tathimini juu ya Mradi wa Kutokomeza mimba na ndoa za utotoni katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu leo Februari 4, 2021.
Mradi huo unaotekelezwa katika kata ya Busangwa wilayani Kishapu ulianza mwaka 2015 ukiwa na lengo la kuijengea jamii uelewa wa kutambua mila kandamizi zinazochangia mimba na ndoa za utotoni kupitia mikutano ya hadhara kutoa elimu kwa wanajamii kupinga mila potofu zinazochangia mimba na ndoa za utotoni.
Akifungua kikao hicho cha Tathimini Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Ndugu. Joseph Swalala amesema kuwa jamii inayotuzunguka inahitaji elimu ya kutosha juu ya masuala haya hivyo amewaomba shirika la OPE kuendelea kuielimisha jamii juu ya masuala ya kupinga mimba na ndoa za utotoni.
“Nawaomba Shirika la OPE kuendelea na harakati hizi za kuoa elimu kwa jamii juu ya mila kandamizi zinazopelekea mimba na ndoa za utotoni kwa kushirikiana na Maafisa Maendeleo ya Jamii Kata” amesema Swalala.
Akitoa tathimini hiyo Afisa Miradi wa Shirika la OPE, Joseph Kasya amesema kupitia mradi wa Kutokomeza Mimba na Ndoa za Utotoni chini ya Shirika la OPE kuna mafanikio makubwa kwani jamii inatoa taarifa na ushahidi juu ya unyanyasaji wa kijinsia na ukatili kwa watoto pamoja na mimba na ndoa za utotoni. Aidha wazazi na walezi wamepata uelewa mzuri wa malezi ya watoto wao hivyo kupelekea kupungua kwa mimba na ndoa za utotoni.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa OPE, William Pius Shayo amewataka wazazi na walezi kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na dawati la jinsia kuhakikisha kwa pamoja wanasimama kuwalinda watoto ili kuepuka kukatisha ndoto na malengo yao.
“Sisi kama jamii tuna wajibu mkubwa wa kuhakikisha watoto wetu wanatimiza ndoto zao kwa kupinga mila kandamizi zinazopelekea mimba na ndoa za utotoni hivyo tuendelee kushirikiana kwa pamoja kutekeleza hilo. Pia natoa shukrani zangu kwa ofisi ya mkurugenzi kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na dawati la jinsia kwa ushirikiano mkubwa wanaoendelea kutupatia” amesema Shayo.
Akihitimisha kikao hicho cha tathimini Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu amepongeza Shirika la OPE kwa kazi wanayoifanya ya kuhakikisha mimba na ndoa za utotoni katika wilaya yetu zinatoweka na kusisitiza walezi na Afisa Maendeleo ya Jamii ngazi ya kata kufuatilia maendeleo ya ‘clubs’ mashuleni ili kuwapa elimu juu ya madhara ya mimba na ndoa za utotoni.
Halmashauri ya Wilaya Kishapu
Anwani ya Posta: S.L.P. 1288 KISHAPU
Simu ya mezani: +255282770020
Simu:
Barua pepe: info@kishapudc.go.tz/ded.kishapudc@shinyanga.go.tz
Hakimiliki © 2016 Halmashauri ya wilaya ya Kishapu. Haki zote zimehifadhiwa